Biteko: Uwepo wa rasilimali madini uwe chanzo cha kujenga viwanda

NA TITO MSELEM-WM

IMEELEZWA kuwa, kiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ni kuona Sekta ya Madini inavutia uwekezaji ili kuhakikisha uanzishwaji wa viwanda kupitia sekta hiyo.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko wakati akifungua mafunzo ya siku nne kwa wachimbaji wadogo wa madini wa Mkoa wa Mwanza ya namna bora ya Uchukuaji wa Sampuli za Uchunguzi na Uchenjuaji wa Madini yaliyoandaliwa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

Ufunguzi huo umefanyika leo Novemba 27, 2021 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wenye lengo la kuwawezesha wachimbaji wadogo kuchimbah kwa tija na waachane na uchimbaji wa kubahatisha.
Waziri Biteko amewataka wachimbaji wadogo wa madini kuyafuatilia maelekezo yote watakayopewa na Taasisi ya GST katika mafunzo hayo ambayo yatawafaa katika shughuli zao za uzalishaji madini na kuongeza tija katika Uchukuaji wa Sampuli za Uchunguzi na Uchenjuaji wa Madini.
Aidha, Waziri Biteko ameipongeza Taasisi ya GST kwa kuandaa mafunzo hayo ambapo amesema GST imekwisha kutoa mafunzo kama hayo katika mikoa 10 ili kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo wa madini nchini katika kuboresha shughuli zao.

“Watu wanaungana ili wafanye shughuli zao kwa ufanisi na mwisho wa siku shuguli zao ziwe na tija, lakini kwa wachimbaji wadogo wa Tanzania wanaungana ili washughulikiane, hapana hiyo sio sawa, pendaneni, thaminianeni na heshimianeni acheni kufitiniana,” amesema Waziri Biteko.
Waziri Biteko amesema Taasisi ya GST ilikuwa Dodoma peke yake lakini sasa hivi imesogeza huduma zake kwa wachimbaji wadogo ili waitumie taasisi hiyo kuwasaidia kubaini namna bora ya uchimbaji, uchenjuaji na ukusanyaji wa sampuli za uchunguzi wa madini.
Sambamba na hilo, Waziri Biteko ametembelea Soko Kuu Kimataifa la Madini-Mwanza ambapo amekutana na wafanyabiashara wa madini ili kusikiliza kero zao na kuzitolea ufumbuzi pia, amewapongeza wafanyabiashara hao kwa kuhamia katika soko jipya la madini lililopo katika eneo la Sabasaba ndani ya kiwanda cha kusafisha madini ya dhahabu cha Mwanza Precious Matals Gold Refinery.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Dkt. Mussa Budeba amewataka wachimbaji wadogo wa madini kuhakikisha wanahudhuria siku zote nne za mafunzo hayo ambapo siku moja imetengwa maalumu kwa ajili ya kujifunza nadharia na siku tatu watajifunza kwa vitendo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news