NA MWANDISHI MAALUM
BODI ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko nchini (CPB) imeingia makubaliano na Kampuni ya Twiga Foods Limited ya Kenya ili kufanya biashara ya pamoja katika soko la Kenya kwenye mazao ya nafaka yakiwemo mahindi na mchele.
Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), Dkt. Anselm Moshi (aliyevaa tai) akipata maelezo kutoka kwa mtalaam wa teknolojia kutoka Kampuni ya Twiga Foods Limited jijini Nairobi nchini Kenya, alipotembelea kuona na kujiridhisha uwezo wa kampuni hiyo wa kusambaza nafaka kabla ya kuingia mkataba wa uuzaji mazao ya bodi hivi karibuni, katikati ni Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Bw. Yebeltal Getachew. (NA MPIGAPICHA MAALUM).
Makubaliano hayo ni matunda ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini humo Mei 6, 2021 ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kufungua milango na kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizi mbili.
Katika kila fursa aliyopata kuzungumza, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa mataifa hayo mawili Kenya na Tanzania kushirikiana bila kuwepo ushindani,kauli au vitendo vya kukwazana.
Kabla ya makubaliano hayo,Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), Dkt. Anselm Moshi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha mahusiano ya Kidiplomasia na nchi mbalimbali ambapo mahusiano hayo yameimarisha biashara kati ya bodi na wafanyabiashara mbalimbali wa nchi hizo.
Dkt.Moshi amesema, bodi hiyo imeingia makubaliano na Kampuni ya Twiga Foods Limited ya Kenya ambapo yanafungua ukurasa mpya katika soko la nafaka kati ya Kenya na Tanzania ili kuleta tija kwa wakulima na wazalishaji wa nafaka hasa kwa Tanzania ambao wanazalisha kwa wingi kwa Ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Twiga Foods Limited ya Kenya, Bw.Yabeltal Getachew, Dkt. Moshi amesema, Bodi ya Mazao Mchanganyiko Tanzania imeendelea kupanua wigo wa masoko kwa kufanya kazi na wafanyabiashara mbalimbali katika Ukanda wa Afrika Mashariki ili kujenga soko imara kwa wazalishaji wa mazao ya nafaka nchini.
“Nimefanya ziara hii ya kikazi jijini Nairobi nchini Kenya katika jitihada za kupanua masoko ya mazao ya wakulima wetu kule Tanzania na lengo la kutembelea Kampuni ya Twiga Foods Limited ni kufanya mazungumzo nao na kujenga msingi wa kibiashara kati ya nchi zetu mbili ili wakulima wetu wasihangaike kutafuta masoko ya kuuza mazao yao,”amesema Bw.Moshi.
Ameongeza kwamba, wamekwenda nchini Kenya kwa mwaliko wa Kampuni ya Twiga Foods Limited ili kuona miundombinu waliyokuwa nayo kwa ajili ya kupokea, kuhifadhi na kusambaza nafaka ambazo zinazalishwa na Bodi ya Mazao Mchanganyiko nchini Tanzania, ambapo kumekuwa na mazungumzo ya muda mrefu,lakini hatimaye umefika wakati wa kusaini mkataba wa ushirikiano.
Aidha, Dkt. Moshi amefafanua kuwa, kampuni hiyo inayo miundombinu ya kisasa kwa ajili ya kupokea, kuhifadhi na kusambaza nafaka, zikiwemo roboti mbalimbali, "jambo ambalo limetuvutia kufanya nao kazi tukiamini kwamba kutakuwa na ufanisi mkubwa katika ushirikiano huu,"ameongeza.
Amesema, Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuzalisha nafaka na mazao mengine ya mikunde, mtama,mazao ya mbogamboga, mazao ya matunda na maua hivyo ameahidi kwamba watafanya nao kazi kwa manufaa ya nchi zote mbili.
“Jambo kubwa ambalo wao wamelieleza ni kumfikishia mlaji chakula kwa bei nafuu zaidi na kwa mtazamo wetu hili ni jambo muhimu sana, kwamba mlaji aweze kupata chakula kwa bei nafuu na kiasi kingine cha fedha zake akitumie katika shughuli za maendeleo,”amesema Dkt.Moshi.
Dkt. Moshi amefafanua kuwa, katika nchi zetu hizi za Kiafrika uzalishaji wa chakula unafanywa na wakulima wadogowadogo hivyo kuna haja ya kuwekeza kwa wakulima wadogo ili kuwasaidia waweze kujikwamua kiuchumi, kwa kuwaunganisha pamoja katika vikundi, au vyama vya ushirika waweze kuzalisha kwa tija na kupata mazao mengi, lakini pia kuuza kwa bei nafuu, ambapo kwa Tanzania limewezekana kwa kiasi kikubwa.
“Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko tutashirikiana na wenzetu ambao tayari wao wana mtandao mkubwa wa masoko ili kuwaunganisha wakulima wetu na kuingia nao mikataba ambayo itawawezesha kuuza mazao yao bila tatizo mara baada ya kuzalisha,”ameongeza Dkt. Moshi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Twiga Foods Limited,Bw. Yebeltal Getachew amesema, amefurahishwa na ujio wa Mkurugenzi wa Bodi na kwamba wako tayari kufanya biashara na bodi hiyo, kwa kuwa wana uhakika wa kupata bidhaa kwa wakati na ubora unaohitajika kwa wakati.
"Sisi na Tanzania ni ndugu, mimi mwenyewe nimewahi kuishi Tanzania na tunasambaza baadhi ya chakula kutoka Tanzania, hivyo natazamia kufanya kazi na bodi kwa karibu sana kwa manufaa ya wananchi na nchi zote mbili kwa ujumla,"amesema Bw. Getachew.