NA MWANDISHI DIRAMAKINI
UMOJA wa Machifu Mkoa wa Singida umewaomba wana umoja huo kufanya zoezi la kuwasimika machifu wengine katika maeneo yao kabla ya kwenda kushiriki mkutano mkuu wa machifu Tanzania utakaofanyika mkoani Kilimanjaro.
Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Mkoa wa Singida, Chifu Mjengi Gwau ameyasema hayo wakati akizungumza katika hafla ya kumsimika Mkuu wa Machifu Mkoa wa Singida, Chifu Mugenyi Senge Mugenyi Ndovu.
Pia amewataka kushirikiana ili kutimiza malengo huku akitoa rai ya kuundwa kwa mabaraza ya wazee watakaosimamia mila na desturi za Kitemi mkoani hapa.
"Na wengine wote tusaidiane ili wafanye haya, tunangojwa kwenda kufanya mkutano wa Umoja wa Machifu Tanzania huko Marangu, Moshi ili tuchague viongozi wa umoja wa machifu, tukishamaliza Chifu Hangaya anatuita machifu wote Dodoma, halafu tutaunda mabaraza ya wazee yatakayosimamia mila na desturi zetu,"amesema Chifu Mjengi.
Aidha, baada ya kusimikwa kuwa Mkuu wa Machifu Mkoa wa Singida, Chifu Mugenyi Senge Mugenye Ndovu ameshukuru kupata nafasi hiyo na kueleza kuwa atakuwa ni kiunganishi kati ya Serikali na jamii katika kufanikisha mambo mbalimbali ya kimaendeleo.
Pia kuhusu migogoro ya ardhi, chifu huyo ameeleza namna ambavyo umilikishaji usiohalali unavyopelekea migogoro na kuiomba Serikali kushirikiana katika kuitatua huku akitoa shukurani kwa Mkuu wa Machifu Tanzania, Chifu Hangaya ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
"Kuna baadhi ya watu ambao wametoka katika mikoa mingine wametumia njia za ujanja ujanja kumiliki maeneo makubwa ya ardhi.
Kwa upande wake, Katibu wa Chifu Ndovu amabaye pia ni mtoto wake, Salum Mghenyi Ndovu amesema mkuu huyo wa machifu atasimamia maeneo ya asili kama vile misitu na vyanzo vya maji.
"Kuna mambo mengi sana ambayo chifu atayasimamia zamani tulikuwa na maeneo yetu ya asili kama vile msitu, vyanzo vya maji ambayo kwa sasa havizingatiwi sana kuna maagizo alitoa Katibu wa Wizara ya Sanaa Utamaduni, Dkt.Hassan Abbasi kuwa machifu waorodheshe maeneo yao yalikuwa ya kiutawala wa kichifu, hivyo kuna maeneo hapa Singida yanahitaji usimamizi wa chifu na ndio kazi ambayo ataifanya,"amesema Katibu huyo.
Hata hivyo, Mkoa wa Singida una jumla ya machifu sita ambao huongoza shughuli mbalimbali za Kitemi kama mila na desturi ya jamii yao kwa lengo la kuendelea kulinda na kuzitunza.