NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetangaza kuanza kwa mgao wa maji katika Mkoa Dar es Salaam.
Mgao huo unaosababishwa na upungufu wa maji Mto Ruvu ambapo unaanza rasmi leo Jumatatu Novemba 8, 2021 na utadumu kwa saa 12 kulingana na ratiba ya mgao wa eneo husika.
Hayo yamesemwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja leo jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Luhemeja amesema kuwa, mamlaka imeandaa utaratibu wa kuhakikisha hakuna mwananchi anapata shida ya ukosefu wa maji licha ya uwepo wa mgao huo.
“Kwa sasa hali ya Mto Ruvu kwa majuma mawili bado iko palepale ambapo kina cha mto kiko katika mita 1.5 hadi 1.8, kwa upande wa Ruvu Juu kina kipo mita 16 hadi 18, hivyo hali ya mto imeendelea kuimarika, kabla ya changamoto ya kiangazi.
"Mamlaka huwa inazalisha lita Milioni 520 kwa siku, kwa sasa tunazalisha lita Milioni 460 kwa siku, hivyo upungufu wa maji upo kwa asilimia 12,"amesema Mtendaji Mkuu huyo.
Mhandisi Luhemeja ameongeza kuwa, kutokana na ukubwa wa mtandao wa DAWASA wametoa ratiba ya mgao wa upatikanaji wa huduma ambazo zitatolewa kwa wananchi kupitia mifumo ya kimawasiliano ya mamlaka katika ofisi za mikoa ya kihuduma.
"Lengo la kuwa na mgao ni kuhakikisha kila mwananchi anaendelea kupata maji kwa uwiano,"amesema.
Pia amefafanua kuwa, maeneo ambayo hayataathirika na mgawo huo ni pamoja na eneo la Kisarawe, Chalinze, Pugu, Bagamoyo, Oysterbay, Masaki, Mikocheni, Ikulu, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Kikwete (JKCI) na Soko Kuu la Kariakoo.