Diamond Platnumz afunguka, awataka vijana kuwekeza

NA GODFREY NNKO

NASIBU Abdul Juma Issack maarufu kama Diamond Platnumz ameendelea kuwa miongoni mwa wasanii vinara ndani na nje ya Tanzania ambao licha ya kutumia vipaji vyao kuendesha maisha pia ameendelea kuwekeza miradi mingi nchini ambayo inatoa fursa za ajira na kuchangia pato la Taifa.
Staa huyo kwa sasa ameonekana kutoa nguvu kubwa katika uwekezaji wa vitu mbalimbali nchini, lengo likiwa ni kumuwezesha hapo muziki utakapomshinda aweze kuhimili mapato yake na kuendelea kutoa ajira kwa Watanzania wengi.

Siku moja baada ya kuzindua kampuni yake ya michezo ya kubashiri ya Wasafi Bet kwa maana ya Novemba 26, 2021, Diamond Platinumz amefanya mahojiano na BBC na kuainisha mambo mbalimbali;

"Kilichopotea ni ngumu kukirudisha, lakini uzuri angalu nchi zinaanza kufunguka taratibu taratibu, na sisi biashara zetu zinaanza kurejea taratibu taratibu. Na katika kusema, tunamerudisha vipi ni uongo, lakini kuweka misingi sahihi ambayo, nafikiri kesho na kesho kutwa ikitokea mambo kama hayo tena, kusiwe na namna yoyote.

UMEJIFUNZA NINI?

"Siwezi kusema, labda ulikuwa wakati mzuri, Lakini mimi mwenyewe nimekuwa katika mazingira ambayo, tunaiogopa sana kesho.

"Kwa hiyo nilikuwa nasema ikitokea kesho na kesho kutwa siwezi kuimba muziki nitawezaje kuhimili mapato yangu, kwa hiyo kidogo mimi nimewekeza katika vitu mbalimbali ambavyo hata leo nisipoimba muziki au nisipoingiza kwenye muziki, basi ninaweza kuendelea katika mapato.

"Lakini kwa ujumla katika muziki, hii inatufundisha kuwa, vijana wengi au watu mbalimbali lazima tuwekeze. Huu muziki au kiwango cha fedha tunachokipata katika muziki, tutumie kama njia chanya ya kuwekeza katika shughuli mbalimbali, ili kesho na kesho kutwa hata kama tutashindwa kufanya 'show' tuweze kutengeneza riziki kwa njia mbalimbali.

ALIANZIA WAPI?

Mwaka 2007, Diamond Platinumz alionekana mtu wa kawaida ambaye hakuwa na ushawishi, lakini miaka mitatu baadaye kwa maana ya mwaka 2010 nyota yake ilianza kung'ara, hivyo muziki ukaanza kuwa chanzo chake kikuu cha mapato.

CEO huyo wa Wasafi Classic Baby (WCB) licha ya kuwekeza katika vyombo vya habari na miradi mingine, muziki wake umekuwa ukifanya vizuri ndani na nje ya Tanzania.

Kutoka ngoma za Kamwambie, staa huyo alianza kupaa kwa kasi katika muziki huku kila ngoma ambayo amekuwa akiitoa zikiwemo Marry You, Waah,Tetema, Inama, Jeje na nyingine nyingi kama ilivyo hapa chini zikimpaisha zaidi, hivyo kumuongezea mapato;
KWA NINI AMEWEZA?

DIRAMAKINI BLOG imefanya mahojiano na baadhi ya wananchi ambao wamefichua siri ya mafanikio ya Diamond Platinumz, kwa nyakati tofauti wananchi hao wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamesema, mafanikio yake yametokana na ujasiri, kutokata tamaa na kufanya kazi kwa bidii.

"Wakati mwingine unaweza kusema fulani anafanikiwa ka sababu ya jambo hili na lile...lakini ukweli ni kwamba mafanikio ya mtu au riziki yake, Mungu ndiye mtoaji, Diamond Platnumz wakati anaanza kutafuta namna ya kutoboa kimuziki alipitia vikwazo vingi, lakini hakukata tamaa.

"Jamaa aliamua kujitoa mazima mazima, yaani kwa kupiga kazi usiku na mchana,bila kulala na mwisho wa siku kufikia malengo yake ambayo ndiyo yamemuheshimisha hadi hapo alipo, sasa anatoa ajira kwa wengi na wengi wanamtegemea kwa ajili ya kufanikisha ndoto zao,"amesema Julius Amos mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, mbali na biashara ikiwemo miradi aliyowekeza kama vyombo vya habari, Diamond Platnumz inaelezwa anaingiza fedha nyingi kutokana na mitandao kama vile Itunes na Youtube.

Siku za karibuni akizungumza ndani ya Wasafi FM, alieleza kuwa,”Naelewa kuwa kuna njia nyingi za kupata pesa kwenye mitandao na kwa sasa muziki wangu unapatikana kwa platform (majukwaa) karibia zote. Platform inayonilipa zaidi ni apple music,”alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news