NA MWANDISHI MAALUM
TUME ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) ni taasisi ya Serikali iliyoundwa kwa Sheria ya Nguvu za Atomiki Na. 7 ya Mwaka 2003 (Atomic Energy Act No.7 of 2003) inayoipa TAEC mamlaka ya kudhibiti matumizi salama ya mionzi na kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia nyuklia hapa nchini ili kulinda wafanyakazi, wananchi, wagonjwa na mazingira dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi.
TAEC yenye Makao yake Makuu jijini Arusha ina Ofisi za Kanda na Mipaka zipatazo ishirini na saba (29), ambapo Ofisi ya Kanda ya Dar es Salaam ina jumla ya Ofisi ndogo ishirini na tatu (23), hii yote ni katika kuhakikisha udhibiti wa matumizi salama ya mionzi unafanyika kikamilifu sambamba na kuhakikisha TAEC inarahisisha ufanyikaji wa biashara kwa kutoa vyeti vya mionzi kwa wakati.
Hayo yamesemwa na Bw. Peter Ngamilo ambaye ni Afisa Mwandamizi na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania katika Tamasha la Mawasiliano, Utalii, Utamaduni na Maoenesho ya Biashara yanayoendelea katika Viwanja vya Malamala vilivyopo Igoma Jiji la Mwanza.
"Huu ni muendelezo wa utoaji wa elimu kwa wadau na wananchi ambapo sisi TAEC kama taasisi yenye mamlaka ya udhibiti wa mionzi hapa nchini tuna jukumu kubwa la kuhakikisha hatuweki rehani afya na maisha ya watanzania dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi, kwani mionzi ina madhara makubwa ambayo yanaweza kuwa ya muda mfupi au muda mrefu ikitegemeana na kiwango cha mionzi alichokipata muhusika.
"Madhara hayo ni kama vile magonjwa ya saratani, hivyo ushiriki wetu kwenye Tamasha hili ni muhimu sana katika kufikisha elimu kwa watanzania hususani wakazi wa Jiji la Mwanza juu ya majukumu tunayoyatekeleza ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," amesema Bw. Ngamilo.
Bw. Ngamilo amesema kuwa, matumizi ya mionzi ambayo ndio teknolojia ya nyuklia inatumika katika sekta mbalimbali hapa nchini ambazo zina manufaa makubwa katika uchumi na kijamii kama vile Afya, Kilimo, Mifugo, Viwanda, Maji,Utafiti na ujenzi, hivyo katika kuhakikisha usalama wa matumizi hayo, TAEC ina jukumu la kuhakikisha inatoa vibali vya uingizaji, usafirishaji, utumiaji na umiliki wa vyanzo vyote vinavyoingia nchini ili kuhakikisha vyanzo hivyo viko katika ubora unaotakiwa kama ambavyo Sheria ya Tume ya Nguvu za Atomiki na Kanuni zake zinavyoelekeza.
Ngamilo ameenda mbali na kusema kuwa pia majengo yote ambako vyanzo hivyo husimikwa kwa ajili ya kutumika ni lazima yajengwe kwa utaratibu na viwango kama ambavyo sheria imeelekeza ili kuzuia uvujaji wa mionzi na kuweza kusababisha athari kwa wananchi na mazingira.
Bw. Ngamilo ameenda mbali zaidi kwa kusema kuwa, katika kutekeleza usalama wa matumizi ya vyanzo vya mionzi pia watoa huduma wanaotumia vyanzo vya mionzi hapa nchini ni lazima wawe na utaalamu kutoa huduma hiyo ili mwisho wa siku wasije kusababisha madhara makubwa yatokanayo na mionzi.
Na kwa kufanya hivyo, Bw. Ngamilo amesema TAEC hufanya kaguzi za mara kwa mara katika maeneo yote yenye vyanzo vya mionzi kama vile katika vituo vya afya vinavyotoa huduma za uchunguzi na matibabu kwa kutumia X-Ray, CT-Scan, MRI, pia kupima viwango vya mionzi kwenye minara ya simu pamoja na rada za mawasiliano, sehemu za migodi, maeneo yote yenye ujenzi wa mindombinu kama vile kwenye mradi wa ujenzi wa reli ta mwendokasi (SGR).
Maeneo yenye utafiti wa mafuta na gesi, kwenye maeneo utafiti unakofanyika kwa kutumia vyanzo vya mionzi katika kuhakikisha usalama wa wafanyakazi, wagonjwa, wananchi pamoja na mazingira dhidi ya madhara ya mionzi.
Bw.Ngamilo ameongeza kwa kusema pia TAEC hupima uchafuzi wa mionzi kwenye anga na mazingira kwa kutumia kituo maalum walichonacho ambapo kituo hicho huweza kubainika viasili vya mionzi katika anga endapo kutatokea na majaribio ya silaha za kinyuklia sehemu yoyote Duniani, ambapo kituo hicho huweza kuonyesha aina gani ya mionzi iliyopo angani kwa wakati huo na nchi ambayo majaribio hayo yamefanyika, hii yote ni katika kulinda wananchi na kudhibiti matumizi ya mionzi ambayo siyo sahihi
Bw. Ngamilo amebainisha kuwa mpaka sasa matukio yaliyohusisha usafirishaji holela wa vyanzo vya mionzi (illicit traficking) Duniani, na vyanzo hivyo kukamatwa ni idadi ya vyanzo 3068 huku Tanzania ikikamata vyanzo vya mionzi vipatavyo 17 katika miaka ya 1996 na 2019 ambapo idadi kubwa ya vyanzo hivyo vilikamatwa jijini Dar es Salaam.