NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MARA nyingi binadamu huwa na tabia ya kuzoea jambo au hata kulipuuzia hususani linapokuwa si takwa lake au hitaji la wakati huo.
Ndiyo maana mara nyingi,wengi wetu tumekuwa tukisisitizwa sana kula matunda kwa afya, lakini kwa kupuuza au kutoona umuhimu wake tumekuwa tukiyaona matunda kama jambo la kawaida.
Licha ya faida lukuki zilizopo katika ulaji wa nanasi, pia kilimo cha manani ni fursa kubwa ya kuinua uchumi wa jamii na Taifa.
Ukweli ni kwamba, ulaji wa matunda una faida kubwa katika afya zetu, na matunda yamebeba utajiri mkubwa wa vitamini ambazo ni muhimu katika maisha yetu.
Ili kuweza kukuthibitishia hayo leo DIRAMAKINI BLOG inakusogezea faida chache za ulaji wa tunda aina ya nanasi.
NANASI NI NINI?
Unapozungumzia kuhusu nanasi, unalenga moja kwa moja kwenye tunda ambalo lina mifanano ya miiba ambalo huwa linatoa maji matamu.
Maji hayo mara nyingi huwa yanatumika kutengenezea juisi ambayo upendelewa zaidi na rika tofauti tofauti ikiwa ya moto au iliyopoozwa katika jokofu.
JE NIKILA NANASI NINAPATA NINI?
Kwa mujibu wa wataalam wa tiba lishe na afya wanaeleza kuwa, ulaji wa tunda aina ya nanasi umuwezesha mtumiaji kuwa na mmeng’enyo mzuri wa chakula.
Mmeng'enyo huo, huwa unafanyika kwa kisi kikubwa na kwa ufanisi bora, kwani ndani ya nanasi kuna aina protini ambayo huwa inauwezesha mwili kurahisisha kazi ya kumeng’enya chakula kwa ufanisi mzuri.
Mbali na hayo pia kuna faida nyingine ambayo ni kuimarisha mifupa, kwani ndani ya nanasi kuna madini aina ya manganese ambayo ni muhimu katika mwili wa binadamu kwa ajili ya kuimarisha mifupa.
Kupitia ulaji au unywaji wa juisi ya nanasi unapata faida kubwa ya kuifanya mifupa yako iwe imara na iliyokomaa, hivyo kukuondolea hofu ya kuishi maisha ya mashaka kutokana na udhaifu wa mifupa yako.
Wataalamu wa afya wanashauri kuwa, uwe unapata japo juisi kikombe kimoja kwa siku cha juisi ya nanasi au kulila kama lilivyo baada ya kulimenya na matokeo yake utayapata kwa haraka.
Faida nyingine ni pamoja na mlaji wa nanasi kuneemeka kupitia madini na protini kwa wingi ikiwemo Fiber, Potassium, Calcium, Vitamin A na Vitamin C. Vitamini hizo mfano C ni muhimu katika mwili wa bianadamu kwani, umuwezesha kukabiliana na baridi na kikohozi.
Pia linautajiri wa Bromelain ambayo uwezesha kudhoofisha virusi vya mafua, ndiyo maana unashauriwa muda wowote ujiwekee utaratibu wa kula tunda hilo.
Wakati unaumwa kula tunda la nanasi hata wakati unakuwa kwenye dozi ya dawa ambazo umepewa na daktari linaweza kukusaidia sana kuharakisha kupona haraka kutokana na utajiri wa vitamini.
Pia ulaji wa nanasi unawezesha kuimarisha meno, ndiyo maana kama una matatizo ya meno au upo imara basi unashauriwa kula nanasi kwa sababu nanasi linasaidia kuimarisha magego ambayo yanashikilia meno ili kuyafanya imara zaidi.
Faida zingine za ulaji wa nanasi ni kupunguza misongo ya mawazo, athari ya ugonjwa wa saratani, kupona haraka baada ya kufanyiwa upasuaji ikiwemo kuboresha na kuimarisha mfumo wa kinga mwilini.
Mbali na hayo, ulaji wa nanasi huwa unazuia ugonjwa wa pumu. Huu ni ugonjwa ambao huathiri sehemu ya kupitisha hewa kwenda kwenye mapafu ya binadamu.
Wataalam wa afya wanasema kuwa, ukijijengea tabia ya kula nanasi unajiweka katika hali nzuri ya kutopata ugonjwa wa pumu. Kwani ndani ya nanasi kuna utajiri mkubwa wa vitamin aina ya Beta Carotene ambayo huwa inausaidia mwili kukabiliana na magonjwa mbalimbali ikiwemo pumu.