NA GODFREY NNKO
André Morgan Rami Ayew (Dede Ayew) raia wa Ghana anayechezea Al Sadd SC ya Qatar ameiwezesha timu yake ya Taifa ya Ghana kusonga mbele kuelekea kufuzu Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.
Bao pekee la winga huyo ndani ya dakika ya 33 ambalo lilipatikana kwa mkwaju ndilo lililozamisha matumaini ya Afrika Kusini kusonga mbele katika michuano hiyo ya Kombe la Dunia 2022.
Ni baada ya Black Stars ambayo ni timu ya Taifa nchini Ghana kuichapa Bafana Bafana ya Afrika Kusini waliowaalika katika dimba la Cape Coast Sports Stadium Novemba 14, 2021 lililopo mjini Cape Coast, Mkoa wa Kati nchini Ghana.
Ni katika Kundi G ambalo lilikuwa na wababe wa soka barani Afrika ambapo kutokana na ushindi huo, Ghana imeongoza kwa alama 13, ikifuatia nafasi ya pili Afrika Kusini wenye alama 13, nafasi ya tatu ni Ethiopia yenye alama tano huku Zimbabwe ikiburuza mkia kwa alama 2.
Aidha, mkwaju huo wa penalti wa kipindi hicho cha kwanza kutoka kwa Andre Ayew umethibitisha kuwa lilikuwa ni goli gumu ambalo limepatikana kwa faida kubwa, huku Ghana wakimaliza kileleni mwa Kundi G.
Ghana ambayo haijawahi kupoteza mechi katika dimba la Cape Coast Sports Stadium tangu 2009 ilimaliza kileleni ikiwa na alama 13, alama sawa na Afrika Kusini. Lakini wao wanarekodi bora ya kufunga mabao.
Kwa ushindi huo, Ghana inaungana na Mali, Misri, Senegal, Morocco na DR Congo. Aidha, washindi hao, wataingia hatua ya mtoano ambapo ni hatua ya mwisho ya kuwania tiketi ya Qatar 2022.
Baada ya mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla, atapatikana mmoja kati ya wawakilishi watano wa Afrika Kombe la Dunia 2022 huko Qatar.