NA LUCAS RAPHAEL
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora imetoa kiasi cha shilingi milioni 240 ya asilimia 10 kwa ajili ya mkopo kwa wanawake,vijana na watu wenye walemavu.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dkt.Batlida Buriani aliyejifunga kitambaa kichwani huku akiwa ameshikilia mkasi akikata utepe na kuwakabidhi watendaji na wasiriamali pikipiki hizo kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Paul Matiko Chacha.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Jerry Mwanga alitoa kauli hiyo kwenye uzinduzi wa soko la mazao ya nyuki,utoaji mikopo kwa vikundi vya wajariliamali na kukabidhi pikipiki kwa watendaji wa kata katika ukumbi wa Flangenge wilayani humo.
Amesema, fedha zilizotolewa na Halmashauri ya Kaliua zinawawezesha wanawake, vijana na walemavu kiuchumi katika wilaya hiyo ambapo ina vikundi 826 vyenye wanachama 8,820.
Mkurugenzi huyo amesema kwamba, kutokana na ufinyu wa fedha zinazopatikana katika halmashauri ina uwezo wa kutoa mikopo kwa vikundi 45 vya wajasiriamali.
Aidha, Mkurugenzi huyo alibainisha kwamba kwa upande wa kuwezesha vikundi vya vijana halmashuari ina uwezo wa kutoa fedha za mikopo kwa vikundi 33 kati ya vikundi 128 kwa mwaka sawa na asilimia 35 na walemavu vikundi 10 kwa mwaka kati ya mahitaji ya vikundi 20 sawa na asilimia 2.
Jerry amesema kwamba,sekta ya maendeleo ya jamii ambayo ikitumika vizuri inaweza kuleta mabadiliko chanja na kwa haraka kwa jamii nzima.
Wakati huo huo Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo alitoa pikipiki 40 kwa wajasiriamali 15 na watendaji kata 35 zenye thamani ya shilingi milioni 69 kwa ajili kuwawezesha kufanyakazi zao vizuri.
Hata hivyo, amesema halmashauri hiyo katika jitihada na mikakati zaidi inahitajika ili kuwa na uwezo wa kukopesha vikundi vingi ili kupunguza tatizo la ajira na kuwainua kiuchumi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Batlida Buriani aliwataka wajasiriamali wote waliopata fedha za mkopo kutoka katika halmashauri hiyo wawahi kurejesha kwa kufuata maelekezo waliopewa ili na watu wengine wenye sifa waweze kupatiwa ili kutekeleza agizo la Rais.
Balozi huyo amesema ili kuwa mwaminifu katika serikali yetu hasa inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa mujibu wa sheria warejeshe haraka marejesho yao bila kufuatiliwa na halmashauri na kufikishwa mahakamani.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dkt.Batlida Buriani akiwa ameshilia mfano wa hundi kwa ajili ya kuwapatia wajasiriamali wa Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora.
Amesema wajasiriamali wadogo wote waliopata fedha za mkopo na makatibu kata waliopata pikipiki hizo wafuate sheria na maelekezo waliopewa na sio kukiuka watapoteza sifa za kuaminiwa na serikali.
Naye mjasiriamali wa vikundi vya Madinda Pure Honey, Paul Madinda ambaye anajishughulisha na uuza asali ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapatia mikopo hiyo ambayo itawasaidia kuinuka kiuchumi.