NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MATUKIO ya ajali za moto nchini yameendelea kuwa kikwanzo ambapo katika tukio la kusikitisha, hoteli nne za kitalii zimeteketea kwa moto huku wageni na wafanyakazi wa hoteli hizo wakinusurika kifo jijini Zanzibar.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Suleiman Hassan amesema hoteli tatu kati ya hizo zimeteketea kabisa na hakuna kitu ambacho kimeokolewa isipokuwa wageni waliokuwa ndani ya hoteli hizo.
“Moto huo ulianza kuteketeza Hoteli ya Villa de Coco na kisha ukasambaa katika hoteli zengine ambazo zipo karibu na hoteli hiyo,” amesema.
Hoteli nyingine ni Spice Island ambayo imeungua vyumba sita vya kulala wageni, Fun Beach na Cobe ambazo zimeteketea zote na wageni wake waliharakishwa kutolewa na kuhifadhiwa katika hoteli zingine.
Kamanda Hassan amesema chanzo chake bado hakijajulikana, lakini taarifa za awali inadaiwa kuwa ni hitilafu za jiko katika hoteli ya Villa de Coco.
Aidha, kwa mujibu wa Kamanda huyo, hoteli hizo zinamilikiwa na wamiliki tofauti ambao ni rai wa kigeni.