NA GODFREY NNKO
WIZARA ya Kilimo imewaeleza wadau mbalimbali wa zao la parachichi nchini kuwa, Mamlaka za Afya na Mimea nchini India zimeruhusu kwa mara ya kwanza kusafirisha parachichi kutoka Tanzania kwenda India.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa kwa umma Novemba 29, 2021 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Kilimo,Bw.Hundson Kamoga.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, India imetoa ruhusa hiyo kupitia taarifa iliyotolewa katika Gazeti la India Na.S.O.4870 (E) ya Novemba 25,2021.
"Wizara ya Kilimo inayo furaha kwataarifu wadau wa zao la parachichi kuwa, Mamlaka za Afya ya Mimea India kupitia Notice (taarifa) Na.S.O.4870 (E) ya Gazeti la India ya tarehe 25, Novemba 2021, imeruhusu kwa mara ya kwanza kusafirisha parachichi toka Tanzania kwenda India.
"Wizara inawashukuru wadau wote walioshiriki katika kufanikisha kufunguliwa kwa soko hili, ikiwemo wataalamu wa zao la parachichi nchini
"Pia tunawashukuru Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ambao walikuwa washirika wetu wakubwa katika mchakato huu,"amefafanua Bw.Kamoga.