GAUTEG-Manuel Chang aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Msumbiji ambaye kwa sasa ameshikiliwa nchini Afrika Kusini anatarajiwa kusafirishwa kwenda nchini Marekani ili kukabiliana na mashitaka ya kashfa ya dola bilioni mbili.
Mheshimiwa Chang alikuwa anashikiliwa Afrika Kusini toka mwaka 2018 kwa maombi ya Serikali ya Marekani kwa madai ya kuhusika katika deni kubwa ambalo lilikuwa limefichwa.
Kashfa hiyo ambayo ilifichuka kuhusiana na mkopo ambao ulitoweka ukiwa na lengo la kuboresha taifa la Msumbiji, uligeuka na kuwa msukosuko mkubwa wa kifedha na kusababisha maelfu ya watu kuingia katika umaskini.
Jaji wa Mahakama Kuu Gauteg ya Afrika Kusini, Margaret Victor amesema, Manuel Chang atakabidhiwa na kusafirishwa kwenda Marekani kukabiliana na mashitaka yanayomkabili.
Awali Mheshimiwa Chang alinaswa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa OR Tambo, ambapo alikuwa akielekea Dubai.
Tags
Kimataifa