NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma wameripotiwa kugoma kulipia huduma ya maji kwa kile wanachodai kuwa bidhaa hiyo inaletwa na Mungu.
Akizungumza katika mkutano wa nusu mwaka wa Wakala wa Usabazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Kigoma, Meneja wa wakala huo wilayani humo, Mhandisi Leo Respicius amesema, tabia hiyo imechangia kupungua kwa mapato yanayotokana na huduma ya maji katika baadhi ya vijiji.
Aidha, kutokana na changamoto hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Ester Mahawe ameitaka RUWASA kushirikiana na viongozi wa vijiji wilayani humo ili kuwaelimisha zaidi wananchi juu ya umuhimu wa kulipia huduma ya maji.
Vijiji vya Mkongoro, Kaseke, Nyamoli na Kidahawe ndipo ambapo baadhi ya wakazi wake wanadaiwa kugoma kulipia huduma hiyo kwa madai maji yameletwa na Mungu.