NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, Leopards imefifisha matumaini makubwa ya Taifa Stars kufuzu hatua ya mtoano kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Qatar.
DRC imewachapa mabao matatu kwa sufuri wakiwa nyumbani katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.
Katika mtanange huo uliopigwa leo Novemba 11,2021 Leopards wameondoka na alama tatu baada ya kiungo wa Lille ya Ufaransa, Gael Romeo Kakuta Mambenga ndani ya dakika ya sita kuipatia timu hiyo bao.
Huku beki wa Cape Town City ya Afrika Kusini, Nathan Idumba Fasika na mshambuliaji wa Sharjah ya Dubai, Ben Malango Ngita dakika ya 85 wakifunga hesabu.
Leopards kwa matokeo hayo inapanda kileleni mwa Kundi J ikiizidi alama moja Taifa Stars kuelekea mechi za mwisho Jumapili hii.
Wakati huo huo, mechi nyingine ya Kundi hilo inachezwa baina ya wenyeji, Benin wenye alama saba pia na Madagascar yenye alama tatu Uwanja wa l'Amitié mjini Cotonou.
Aidha, kundi limezidi kuwa gumu kwa sababu timu yoyote inaweza kusonga mbele.
Ni kwa kuwa, Madagascar wakishinda mechi mbili za mwisho watamaliza na alama tisa na Taifa Stars inaweza kufuzu ikishinda mechi ya mwisho na endapo Benin na DRC zitatoa sare Jumapili hii huko DRC.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hivi karibuni ametoa wito kwa Watanzania pamoja na wadau wa soka nchini kuungana kwa pamoja na kuhakikisha Taifa Stars inafanya vizuri kwenye michezo yote iliyobaki ili kufuzu kushiriki kombe la Dunia litakalofanyika nchini Qatar 2022.
Alitoa wito huo Novemba 4, 2021 wakati akiongoza kikao cha pamoja cha wadau wa soka nchini katika ukumbi wa uwanja wa Taifa wa Uhuru, jijini Dar es Salaam. Ambapo katika kikao hicho wadau wa Taifa Star wamechangia Shilingi Bilioni 1.6 ambazo zitatumika kuihudumia timu katika maandalizi ya mechi zilizobaki za kufuzu kombe la Dunia.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mheshimiwa Majaliwa amesema ni lengo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha anakuza sekta ya michezo nchini na anataka kuona mafanikio katika timu za Taifa hivyo mikakati ya kuifanya timu ya Taifa ifanikiwe ni sehemu ya kutimiza malengo ya Mheshimiwa Rais.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda, taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wengine kuendelea kujitokeza kuichangia timu ya Taifa ili iweze kuweka Historia ya kushiriki kombe la dunia kwa mara ya kwanza.
Wadau Walioshiriki katika kikao hicho ni pamoja na GSM, TAIFA GAS, AZAM, CRDB, NBC, LAKE OIL, STAR OIL, K4 SECURITY, KAMBIASO pamoja na wadau wengine.
Tags
Michezo