NA GODFREY NNKO
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeingia kwenye mkataba wa miaka miwili na Kampuni ya GSM Group wenye thamani ya shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya kuidhamini Ligi Kuu Tanzania Bara.
GSM Group ameingia kwenye huo mkataba kama mdhamini mweza wa Kampuni ya NBC ambayo awali iliingia mkataba na TFF wa miaka mitatu kwa ajili ya kuidhamini Ligi baada ya Kampuni ya Simu ya Vodacom kujiondoa.
Mkataba huo, umesainiwa mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani na Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Group, Mhandisi Hersi Said.
Hafla hiyo imefanyika jijini Dar es Salaam Novemba 23, 2021 ambapo kwa pamoja viongozi hao wameonyesha mfano wa hundi mbele ya waandishi wa habari.
Makamu wa Kwanza wa Rais TFF, Athuman Nyamlani (Kulia) na Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Group, Mhandisi Hersi Said (kushoto) wakionesha mfano wa Hundi ya mkataba uliosainiwa wa Udhamini Mwenza wa Ligi Kuu Tanzania Bara wenye thamani ya shilingi Bilioni 2.1 kwa miaka miwili.
Makamu wa Kwanza wa Rais, Nyamlani akizungumza kwa niaba ya Rais wa TFF amesema, ni wakati sasa wa kuachana na baadhi ya mizaha ambayo haina afya katika soka letu, badala yake tujikite kuhamasisha wadau wengine kuwekeza katika soka kwa matokeo makubwa zaidi.
Naye Hersi Said amesema, mbali na kuidhamini Yanga, Coastal Union na Namungo udhamini wa sasa umekuwa bora na wenye lengo la kuona ushindani zaidi kwenye ligi ilikuwa na ligi bora na baadaye kuwa na timu ya taifa nzuri ambayo italeta matokeo ya haraka.