Maagizo ya Rais Dkt.Mwinyi kwa viongozi kuhusu ripoti ya CAG

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka viongozi na watendaji wa wizara na idara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutekeleza wajibu wao katika kusimamia mifumo ya ukusanyaji na matumizi ya fedha za Serikali, huku akibainisha kuwa Serikali haitegemei ripoti ijayo ya mwezi Juni, 2022 kusheheni rundo la dosari.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara za SMZ baada ya kukabidhiwa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar Novemba 11, 2021. (Picha na Ikulu).

Dkt. Mwinyi ametoa maagizo hayo Novemba 11, 2021 Ikulu jijini Zanzibar baada ya kupokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).

Ni katika hafla ambayo ilihudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla, mawaziri pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema, viongozi na watendaji hao wana wajibu wa kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika kusimamia mifumo ya ukusanyaji na matumizi ya fedha, huku akionya endapo ripoti ijayo itafanana na ile iliowasilishwa kwake hii leo, itamaanisha bado Viongozi na Watendaji hao hawajachukua hatua zinazostahili.

Alisema, suala la Bajeti ni muhimu katika kutekeleza mipango ya Serikali na kusisitiza kuwa hilo sio jukumu la CAG pekee bali ni la Viongozi na Watendaji wote. Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu wa Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakifuatilia Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Dkt.Othman Abass Ali.(hayupo pichani) akiwasilisha ripoti hiyo kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.(Picha na Ikulu). Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Haroun Ali Suleiman na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Mhe.Jamal Kassim Ali, wakifuatilia Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Dkt. Othman Abass Ali.(hayupo pichani) akiwasilisha ripoti hiyo, hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu). 

Amesema, kila mmoja ana wajibu wa kurekebisha hali hiyo na kusema malalamiko mengine yanayotolewa na watendaji hao hayazingatii wajibu walionao katika kusimamia makusanyo na matumizi ya fedha za umma.

Amesema, ripoti iliyowasilishwa imebainisha kuwa fedha nyingi zinazopaswa kuingia Serikalini haziingii.

Dkt. Mwinyi amekumbusha umuhimu wa watendaji hao kutembelea taasisi zao ili kuhakikisha zinatekeleza wajibu wake , ikiwemo wa ukusanyaji wa mapato pamoja na matumizi yake huku akisisitiza kwamba mfumo wa kutoa taarifa za (CAG) hadharani utaendea ili wananchi waweze kupata taarifa.

Nae, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Dkt. Othman Abass Ali akiwasilisha Muendelezo wa Ripoti ya Ukaguzi wa Mfumo wa usimamaizi wa Fedha, ikiwa ni maagizo yake ya kurejewa ukaguzi huo. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar, Dkt. Othman Abass Ali akizungumza na kuwasilisha Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali, kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) hafla hiyo iliofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar ambapo ulihudhuriwa na Mawaziri na Makatibu Wakuu.(Picha na Ikulu).

Amesema, taarifa za ukaguzi huo ni wa miaka mitano, lengo ikiwa ni kuhakikisha kunakuwepo udhibiti mzuri wa fedha na kubainisha dosari kadhaa zilizobainika, ikiwemo ile ya taarifa za hesabu za hazina kutokuunganishwa na mfumo kwa maana ya kuwa hesabu hizo zimerikodiwa kwa mkono ‘manual’ katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na Benki ya wananachi wa Watu wa Zanzibar (PBZ).

Amesema athari kubwa ya matumizi ya mfumo huo Manual ni kutoa fursa ya kufanyika matumzii yasio rasmi au matumizi holela.

Amesema, changamoto nyengine ni ya kuwepo kwa Hesabu za Wizara, Idara na Wakala wa Serikali ambazo nazo hazikuunganishwa na mfumo na hivyo Idara hizo kukusanya mapato na kurekodi kwa njia ya mkono.

Dkt. Abass amesema dosari nyingine ni kutokuwepo taarifa za ujumuishi wa mwisho wa mwaka (Juni) ambapo hesabu hufungwa, ambapo ukaguzi umebaini kuwepo fedha nyingi zilizobaki katika madaftari ya Wizara na taasisi husika, lakini kukosekana kabisa fedha hizo Benki.

Akitoa mfano wa mwaka 2019 amesema, katika vitabu vya taasisi ilionyesha serikali ilikuwa na Bakaa ya Shilingi Bilioni 1.2 lakini Benki hakukuwa na fedha kabisa. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Dkt. Othman Abass Ali, hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu taarifa za taasisi zilionyesha kuwepo bakaa la shiligni Bilioni 39.713 lakini hakukuwa na fedha yoyote Benki na kusema katika Huduma za Mfuko Mkuu, hali ilikuwa hiyo hiyo.

Alisema endapo maamuzi yalifikiwa ya kutumia mfumo wa Manual, basi ilipaswa kuhakikisha kiwango cha fedha zitakazobainishwa katika vitabu hivyo inalingane na fedha zilioko Benki, jambo ambalo ni tofauti.

Katika hatua nyengine, CAG alieleza taarifa ya ukaguzi maalum wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Kizimbani akiwa ni agizo alililitoa Rais katika ziara yake mnamo Jai 8,mwaka huu wakati akitembelea miradi mbali mbali ya maendeleo huko Dole, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo alibainisha dosari kadhaa zilizojitokeza katika ukaguzi wake ikiwemo kukosekana kwa muongozo wa ukusanyaji wa mapato ya taasisi hiyo.

Alisema ukaguzi uimebaini kukosekana kwa muongozo wa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na shughuli za Utalii pamoja na uuzaji wa miche, mazao pamoja na ukodishaji wa mashamba ya taasisi.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Zanzibar.Mhe. Haroun Ali Suleiman, wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) akizungumza baada ya kukabidhiwa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.Dkt.Othman Abass Ali, hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Alieleza kubainika utofauti mkubwa kati ya makadirio na makusanyo ya mapato, watumishi kufanya kazi kinyume na mikataba ya ajira zao pamoja na dosari katika ukodishaji wa miti ya mazao kwa kutofanyiwa tathmini za awali.

Aidha, alisema ukaguzi huo umebaini kuwepo dosari ya kutoidhinishwa kwa ada na Tozo nyengine kwa mujibu wa taratibu pamoja na upotevu wa mapato utokanao na sabau za kutobainishwa kwa vyanzo vya mapato ya taasisi hiyo.

Dkt. Abass alibainisha kasoro nyingine ni ucheleweshaji wa muda mrefu wa kutuma fedha za mapato benki,kutokuwepo Daftari la wageni, kutokuwepo kwa kumbukumbu za miche inayozalishwa na kuuzwa, sambamba na kuwepo Stakabadhi zisizo rasmi (hazina Tin namba wala ZRB namba) pamoja na kuwepo risiti zinazochapishwa na Taasisi bila muongozo wa Serikali.

Vile vile, alisema Ukaguzi umebaini kuwa dosari ya kutokuzisajili tafiti zilizokamilika huikosesha fedha nyingi Serikali, sambamba na kukosekana kwa usajili wa miti ya kudumu na vitalu vya Miche katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

Katika hafla hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, alikabidhi nakala za taarifa hizo kwa Makamo wa Kwanza wa Rais Othman Masoud Othman, Makamo wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla pamoja na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmeid Said.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news