NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amewataka wafanyakazi wa Sekta ya Afya na wananchi kuisaidia Serikali kuokoa fedha kwa kutumia hospitali zalizopo nchini badala ya kwenda kutbiwa katika hospitali za nje ya nchi ambapo hupelekea Serikali kutumia fedha nyingi.
Mheshimiwa Mazrui amesema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mionzi iliyofanyika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, ambapo sherehe hiyo hufanyika kila ifikapo Novemba 8 ya kila mwaka.
Waziri Mazrui amesema, Kituo cha Hospitali Kuu cha Mnazi Mmoja ni kituo cha kujifunzia kwa wataalamu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, kwani sasa kina wataalamu wazuri waliobobea katika taaluma ya afya na vifaa vingi vya kisasa.
Pia aliwasihi madaktari kutowauzia huduma za afya wagonjwa, kwani kufanya hivyo husababisha kupata laana za wangonjwa na kupelekea wananchi kuilaumu Serikali jambo ambalo sio sahihi na ni kinyume na maadili ya kazi.
Vilevile aliwasisitiza madaktari kutovunjika moyo na kufanya kazi kwa moyo mmoja kwani Serikali inatambua kuwepo kwa changamoto ambazo wanakabiliana nazo wataalamu wa Kitengo cha Mionzi katika hospitali mbalimbali .
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dkt. Msafiri Marjani amewaomba wataalamu wa mionzi kuwafikishia wananchi taaluma hii juu ya faida na hasara zinazopatikana katika vipimo hivyo.
Pia aliwataka wananchi kuacha tabia ya kupiga mionzi mara kwa mara bila ya kuwa na tatizo kubwa ambalo litalazimu kufanya vipimo hivyo kama vile EX-RAY na CT SCAN kwani vipimo hivyo vina mionzi mikali ambayo inaweza kusababisha madhara makubwa zaidi kwa wagonjwa.
Nao wataalamu kitengo hicho walieleza kuwa Kituo cha Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kimeweza kupunguza idadi kubwa ya wagonjwa wanofika kwa kupatiwa huduma hiyo kutokana na kuwepo na vituo vya huduma hiyo kila wilaya.
Wafanyakazi hao wameiomba wizara kuwapatia nafasi za kwenda kusoma kozi za muda mfupi ili kuongeza taaluma zaidi kwani elimu inaongezeka kila siku.