Madiwani washtushwa na uvamizi wa kitalu cha uwindaji wa kitali cha Katoto

NA RESPICE SWETU

WAJUMBE wa baraza la madiwani na wataalamu wa idara mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wameshtushwa na uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanyika katika hifadhi ya kitalu cha uwindaji wa kitali cha Katoto kilichopo wilayani humo na kuahidi kukabiliana na uharibifu huo.

Ahadi hiyo wameitoa walipofanya ziara ya kutembelea hifadhi ya kitalu hicho kujionea changamoto zinazopo na kutafuta namna ya kuzitatua.

Akizungumza baada ya kutembelea kitalu hicho mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu, Eliah Kagoma amewataka wajumbe wa baraza hilo, kubuni mikakati itakayowezesha kukabiliana na uharibifu unaofanyika katika maeneo ya kitalu hicho.

"Tumejionea hali halisi ya uharibifu unaofanyika katika kitalu chetu, tukitoka hapa tunakwenda kufanya majumuisho ya ziara hii na kuweka maazimio yatakayohakikisha kuwa kitalu hiki kina lindwa," alisema Kagoma akiwa kitaluni hapo.

Wakati wa ziara hiyo, palishuhudiwa makundi ya n'gombe na kilimo kilichoshamiri jirani na makazi ya swala, pofu, nyemela, ngiri, nyati, tembo, simba, mamba na korongo wanaopatikana katika kitalu hicho hali inayoashiria kupotea kwa kitalu hicho.

Akitoa taarifa kuhusu kitalu hicho, ofisa wanyamapori wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu, Mohamed Omary alisema halmashauri ya wilaya ya Kasulu imekuwa ikinufaika na mapato yatokanayo na kitalu hicho kutokana na gawio la asilimia ishirini na tano kila mwaka kwa uwindaji wa kitalii.

Manufaa megine kwa mujibu wa Omary ni ruzuku ya maendeleo inayopelekwa katika vijiji vilivyopo jirani na kitalu hicho na fidia zitokanazo na uvuvi wa samaki unaofanyika katika mto Malagarasi ulio katika mwambao wa hifadhi hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news