Mahakama yatupa pingamizi la aliyekuwa DC Wilaya ya Tabora

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Shauri mama la madai linalomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Kitwala Komanya akitakiwa kulipa fidia ya shilingi Milioni 140 limepangwa kutajwa Novemba 9,2021 baada ya Mahakama kutupa pingamizi la mdaiwa.

Akihairisha shauri hilo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Tabora, Nzige Sigwa amesema hoja zilizowasilishwa na Wakili wa Mdaiwa zikitaka shauri hilo liondolewe hazina mashiko kisheria.
Hakimu Nzige akitoa maamuzi hayo madogo amesema, Mahakama imejiridhisha kwamba wakili wa mdai, Kelvin Kayaga amefuata taratibu na kanuni zinazohusu mashauri ya madai.

Komanya kupitia kwa Wakili wake, Issa Rajabu Mavulla aliwasailisha pingamizi Mahakamani hapo akitaka shauri hilo liondolewe kwa kile alichodai mlalamikaji Alex Ntonge alishindwa kuanisha madai yake kwa mujibu wa sheria.

Wakili Mavula aliiambia Mahakama hiyo kuwa, hakuna madai ya msingi, hivyo mteja wake ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya wa zamani hawezi kulipa fedha hizo.

Alex Ntonge ambaye ni mdai katika shauri hilo anataka alipwe shilingi milioni 140 kama fidia kutokana na kudhalilishwa pamoja na kufunguliwa kesi ya jinai kwa nia ovu.

Awali Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Tabora, Nzige Sigwa upande wa mdai ukiongozwa na wakili Kayaga ulidai kwamba mdaiwa alimdhalilisha mteja wake Alex Ntonge, Januari 5,2021.

Aliongeza kuwa, siku hiyo mdaiwa Kitwala Komanya ambaye wakati huo alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora akiwa ameambatana na askari wa Jeshi la Polisi walifika nyumbani kwake na kumdhalilisha.

Ilidaiwa kwamba, mdaiwa akiwa na askari wenye silaha baada ya kufika nyumbani hapo walimkamata mdai Alex Ntonge na kisha walimfanyia vitendo vinavyodhalilisha utu wake mbele ya familia yake na majirani zake.

Mdaiwa katika shauri hilo, Kitwala Komanya alienguliwa nafasi ya Mkuu wa Wilaya na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Samia Suluhu Hassan mwezi Juni 19,2021 baada ya kupangua nafasi za wakuu wa wilaya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news