Makamu wa Rais Dkt.Mpango afungua warsha ya 25 ya utafiti ya REPOA

NA MWANDISHI MAALUM

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe leo Novemba 10, 2021 amefungua warsha ya utafiti ya REPOA ya 25 ,warsha ilioandaliwa kwa kushirikiano na Wizara ya Viwanda na Biashara. Warsha hiyo ya mwaka 2021 imebeba dhima ya Mageuzi ya uchumi wa Tanzania kupitia uzalishaji viwandani na biashara shindani.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akiwasili katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam katika ufunguzi wa Warsha ya 25 ya utafiti ya REPOA. Novemba 10,2021.

Akifungua warsha hiyo Makamu wa Rais amesema katika karne ya 21 Taifa haliwezi kupata maendeleo ya haraka pasipo kutumia tafiti kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia mara kwa mara hivyo utoaji maamuzi pamoja na kupanga mipango ya maendeleo kunahitaji kuongozwa na matokeo ya tafiti.

Makamu wa Rais amesema serikali ya awamu ya sita itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa watafiti wa ndani katika kuwawezesha kuzalisha tafiti za sera zenye ubora pamoja na kuwahusisha katika majadiliano wakati wa utungaji wa sera mbalimbali za taifa.

Amesema katika kukuza uchumi shindani serikali ya Tanzania imeendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu, ukuzaji ujuzi pamoja na elimu ya ufundi ili kuendana na mazingira shindani pamoja na ukuaji wa haraka wa teknolojia.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza na washiriki mbalimbali waliohudhuria Warsha ya 25 ya utafiti ya REPOA wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.Novemba 10,2021.

Aidha Makamu wa Rais ameziasa sekta binafsi kuendelea kutoa mchango wao katika kukuza uchumi shindani ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika kuwejengea uwezo vijana ili kuwawezesha kuwa na ufanisi katika kazi .Aidha ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kuendelea kutoa mchango wao katika vipaumbele vya taifa pamoja na kuwasihi watanzania kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uzalendo na uwazi ili kuliletea taifa maendeleo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA Dkt. Donald Mmari amesema warsha hiyo ni muhimu kwa kuwa inatoa nafasi kwa watunga sera na viongozi kusikia matokeo ya tafiti pamoja na uzoefu wa nchi nyingine ili kuhuisha mipango na sera za Tanzania katika kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka zaidi.

Aidha amesema dhima inayotumika katika warsha hiyo inauwiano na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa unaolenga kuimarisha uchumi wa viwanda ili uwe shindani katika kupata masoko , mitaji, pamoja na rasilimali za uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya ajira na ustawi wa wananchi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wabunge wa Baraza la Wawakilishi mara baada ya ufunguzi wa 25 ya utafiti ya REPOA. Novemba 10,2021.

Aidha Dkt. Mmari ameongeza kwamba kutokana na kubadilika kwa teknolojia ya viwandani katika mapinduzi ya nne ya viwanda, tafiti zinaonesha nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania hazina budi kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wenye tija na ajira kwenye sekta za kati pamoja na sekta ndogo zenye uwezo wa kuwa shindani kwa muda mfupi.

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Viwanda na Biashara Prof Kitila Mkumbo amesema serikali inatambua mchango wa taasisi za utafiti hapa nchini na itaendelea kupokea matokea ya tafiti hizo katika kuboresha utendaji serikalini. 

Amesema warsha hiyo itasaidia mpango wa serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara wa kuandaa mpango maalum wa utekelezaji wa sera ya viwanda nchini huku akisisitiza sekta ya viwanda ni muhimu katika uchumi shindani utakaoweza kutoa ajira na kuondoa umasikini kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news