NA GODFREY NNKO
Shirikisho la Riadha Duniani (WA) kwa kushirikiana na Kamati ya Maandalizi (LOC) kwa ajili ya Mbio za Dunia za Nusu Marathoni Yangzhou 2022 wameridhia kuhairisha mashindano hayo ambayo yalitarajiwa kufanyika Yangzhou nchini China mwezi Machi 27, 2022.
Baada ya uamuzi huo, wamelazimika kuyasogeza mbele hadi Novemba 13, 2022 kwa sababu za kiusalama na masharti magumu ya usafiri ya kudhibiti maambukizi ya Virusi Vya Korona (UVIKO-19) nchini China.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirikisho hilo lenye makao yake makuu nchini Monaco, uamuzi huo wameufikia baada ya kuafikiana na kamati ya maandalizi.
“Shirikisho la Riadha Duniani na Kamati ya Maandalizi ya Riadha za Dunia za Nusu Marathoni tumekubaliana kuahirisha mashindano hayo yaliyopaswa kufanyika mjini Yangzhou nchini China mwezi Machi 27, 2022. Kwa sasa yataandaliwa Novemba 13, 2022,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa WA na LOC mjini Yangzhou,wamedhamiria kupanga na kuandaa mashindano ambayo yatakuwa salama na huru kwa wanariadha kutoka mataifa mbalimbali duniani ambapo wataendelea kutoa taarifa zaidi hapo baadae.