Mashindano ya Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania (UMISAVUTA) yaanza Mtwara, Waziri Prof.Ndalichako atoa rai

*Walimu Tarajali zaidi ya 650 washiriki

NA MWANDISHI MAALUM- WyEST

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako amesema kuwa Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo vitasimamiwa ipasavyo ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa michezo shuleni na katika Vyuo vya Ualimu.
Baadhi ya timu zinazoshiriki mashindano ya UMISAVUTA kutoka Kanda mbalimbali zikipita uwanjani kutoa heshima kwa mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo yaliyofanyika mkoani Mtwara Novemba 29, 2021.

Hayo yamesemwa kwa niaba yake Novemba 29, 2021 mkoani Mtwara na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul wakati akifungua mashindano ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania (UMISAVUTA) yanayoendelea mkoani humo hadi Desemba 5, 2021.

Amesema Rais Samia Suluhu alitoa maelekezo ya kuboresha mitaala na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika nyakati tofauti ameagiza kutekelezwa kwa ufundishaji wa masomo ya sanaa na michezo, hivyo Wizara inaendelea kutekeleza maagizo hayo ili kufikia azma ya Serikali ya kuhakikisha vipawa vya wanamichezo na Sanaa vinakuzwa kuanzia shuleni na pia Taifa linakuwa na wananchi wenye nguvu na afya njema kuweza kulitumikia Taifa.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul akiongea na wananchi (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania (UMISAVUTA) uliofanyika mkoani Mtwara Novemba 29, 2021. Mashindano hayo yanaendelea hadi Desemba 5, 2021.

Aidha, katika hatua nyingine Naibu Waziri Gekul amewataka washiriki wote wa mashindano hayo kuhakikisha wanachukua tahadhari zote za maambukizi ya ugonjwa wa Uviko-19 katika kipindi chote cha mashindano hayo, na kuwahimiza kupata chanjo ya ugonjwa huo.

Awali, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe alisema lengo la mashindano hayo ni kukuza na kuendeleza vipaji kwa walimu tarajali ili nao waweze kwenda kukuza vipaji vya wanafunzi katika michezo na sanaa.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe akiongea na wananchi (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania (UMISAVUTA) uliofanyika mkoani Mtwara Novemba 29, 2021. Mashindano hayo yanaendelea hadi Desemba 5, 2021.
Baadhi ya wananchi wakimsikiliza mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Umoja wa Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania (UMISAVUTA) uliofanyika mkoani Mtwara Novemba 29, 2021. Mashindano hayo yanaendelea hadi Desemba 5, 2021.
Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul akipita kukagua timu mbalimbali zinazoshiriki mashindano ya UMISAVUTA yanayoendelea mkoani Mtwara.
Baadhi ya wachezaji wa mpira wa miguu kutoka timu za Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kati wakiwa katika mechi ya kwanza ya mashindano ya UMISAVUTA yanayoendelea mkoani Mtwara hadi Desemba 5, 2021.

Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo amemuhakikishia mgeni rasmi kuwa Wizara itahakikisha mashindano hayo yatafanyika kwa nidhamu na maadili hadi yanapofikia tamati.

Naye Mwenyekiti wa Walimu wa Vyuo vya Ualimu vya Serikali Tanzania Bara, Mwl. Dorothy Mhaiki amesema mashindano hayo yamehusisha wanachuo 665 kutoka vyuo 36 vya ualimu vikiwemo 35 vya Serikali na kimoja binafsi.

Timu za mpira wa miguu kutoka Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kati ndizo zilizofungua dimba la mashindano hayo ambapo timu ya Kanda ya Ziwa iliibuka na ushindi wa mabao 3 – 0.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news