NA GODFREY NNKO
JOACHIM Marunda Kimaryo maarufu kama Master J ambaye ni muandaaji mbobezi katika muziki nchini Tanzania huku akiwa na uzoefu wa miaka mingi amesema kuwa, wanaojiita chawa wa wasanii wakubwa hawasaidii kukuza muziki wa Tanzania badala yake wanaorudisha nyuma.Master J ambaye licha ya kufanya kazi nyingi zenye ubora wa Kimataifa amewahi kupata tuzo ya Kili Music Awards mara mbili, mwaka 2004 na 2006 huku akiwa mmiliki wa studio mbalimbali za muziki.
Ameyasema hayo leo Novemba 22, 2021 wakati akijibu swali la mfuasi wake katika ukurasa wa Facebook anayejiita Yusuph Nanjanga ambaye alitaka kujua faida ya chawa kwa wasanii.
"Mambo vipi Master J? Swali langu ni hili, unawaongeleaje hawa wanaoitwa machawa wa wasanii wakubwa hapa Bongo? Je wanasaidia 'ku push' (kusukuma) mziki wetu au wanachangia kuuvuruga?. Yusuph Nanjanga alimuuliza Master J.
Akiwa miongoni mwa mastaa ambao kwake haoni shida ya kujadiliana jambo lolote na wafuasi wake katika ukurasa wake wa Facebook kwa kila jambo analobandika, Master J alitumia nafasi hiyo kumjibu mfuasi wake ifuatavyo;
"Yusuph Nanjanga kwa mtizamo wangu hawasaidii kukuza muziki wetu ila wanaurudisha nyuma. Hatuwezi kushindana na Wanaigeria au Wasauzi wakati sisi wenyewe hatuna umoja, UMOJA NI NGUVU, KUTENGANA NI UDHAIFU. Hizi ishu za u-team na ugomvi zinawanufaisha wenye kurasa za udaku tu,"amesema.
Kwa nyakati tofauti baadhi ya Watanzania wapenda burudani ya muziki jijini Dar es Salaam wameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, mastaa wanaotumia chawa kufanikisha mipango yao wamekuwa sababu ya kutengeneza chuki na kutengeneza ubinafsi ambao hauna faida kwa tasnia ya muziki nchini.
"Mtu anajiita chawa wa fulani, anatumia mitandao ya kijamii daily (kila siku) kurusha vijembe kwa wengine. Kila linalofanywa na msanii mwingine anayeonekana kupiga hatua wanamrusha madongo ambayo wakati mwingine yanakera na hata kukatisha tamaa. Nionavyo huu uchawa ni kirusi hatari, hatupaswi kuwashabikia hao chawa, hawana faida katika soko la burudani,"amesema Mussa Mussa mkazi wa Kigogo Fresh wakati akizungumza na DIRAMAKINI BLOG.
Irene Thomas ameunga mkono hoja ya Mussa kwa kusema kuwa, pengine huenda hao chawa wanafaidika zaidi katika sanaa kuliko hata wasanii wenyewe.
"Wamezidi kutengeneza bifu ambazo hazina nyuma wala mbele, Inafaa tuwakemee na kuwakataa kabisa, huu ni ushamba, wanaifanya hii tasnia ya muziki ionekane sufuri wakati ni kati ya sekta ambazo ni nzuri na zina faida kubwa katika kutoa burudani, ajira na hata kukuza pato la Taifa,"amesema Thomas katika mahojiano na DIRAMAKINI BLOG akiwa Ilala Boma.