NA HADIJA BAGASHA
MBUNGE wa Jimbo la Korogwe Vijijini, Timotheo Mzava ameihoji Serikali sababu za kushindwa kulimega shamba la mkonge la Mwakinyumbi Estate kwa ajili ya kugawiwa wananchi kufanyia shughuli za kilimo.
Mbunge Mzava ametoa kauli hiyo,wakati akiuliza maswali mawili madogo ya nyongeza akimtaka Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi kuandamana naye hadi kwenye shamba hilo kumaliza kilio cha wananchi wa Korogwe.
Mzava amesema, Wilaya ya Korogwe imezungukwa na mashamba ya Mkonge na Chai na kwamba kwa sasa wananchi hawana maeneo ya kilimo wakati kwenye mashamba hayo maeneo makubwa yameshindwa kuendelezwa.
Mbunge huyo ameitaka serikali kukaa na wawekezaji wa mashamba hayo ili wakubaliane namna wanavyoweza kuipata ardhi ya maeneo ya mashamba hayo ,kumaliza kilio cha vijana ambao ndio wahanga wakubwa wanaokosa maeneo ya kufanyia shughuli zao za kiuchumi.
Akijibu maswali hayo Waziri Lukuvi amekiri kilio cha mbunge huyo kuwa cha muda mrefu huku akiahidi kufikia kwenye utatuzi wa kero hiyo mara tu baada ya kumalizika vikao vya bunge.
Waziri Lukuvi amesema, uchunguzi wa ndani uliofanywa umebaini kuwa shamba hilo limetelekezwa na hakuna uendelezaji wowote uliofanyika huku likidaiwa pango la ardhi kiasi cha shilingi milioni 174 hadi sasa kodi na malimbikizo kwa muda wa miaka 17 kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka huu wa 2021.
Kutokana na hali hiyo serikali ilianza kubadilisha miliki ya shamba husika kwa kutuma ilani ya ubadilisho kwa mmiliki ndani ya siku tisini na mmiliki hakuweza kujibu chochote dhidi ya ilani hiyo.
Lukuvi amesema, baada ya kufikia hatua hiyo serikali kwa sasa inaendelea na hatua ya ubadilisho akitaja hatua hiyo kuwa ni pamoja na kuandika barua kwa Mheshimiwa Rais ambaye ndiye kisheria mwenye nguvu ya kufuta umiliki wa shamba hilo.
Hata hivyo, Lukuvi amesema ufutaji wa hati za mashamba yasiyoendelezwa na zoezi endelevu kwa mujibu wa sheria likiwa na lengo la kulinda maslahi ya Taifa, wananchi na wawekezaji.
Tags
Habari