NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Ndani ya kipindi cha miaka 60 ya Uhuru,Serikali imesema imepata mafanikio 23 katika sekta ya umeme na nishati jadidifu ikiwemo kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme.
Aidha, hadi kufikia Septemba, mwaka huu upatikanaji wa umeme umefikia Megawatts 1,607 ikilinganishwa na Megawatts 17.5 kabla ya Uhuru ambapo nchi nzima ni mikoa miwili tu ndio lilikuwa na umeme ukiwemo wa Tanga na Dar es Salaam.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba ameyasema hayo leo Novemba 9,2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Mheshimiwa Mhandisi Mramba alikuwa akielezea mafanikio na maendeleo ya sekta ya nishati katika miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Amesema,mikoa hiyo ilikuwa na umeme kwa sababu ya shughuli zilizokuwa zikifanyika ambapo Dar es Salaam kulikuwa na Shirika la Reli ya Kati na Tanga kulikuwa na shughuli za kilimo cha mkonge.
Mhandisi Mramba amesema,mahitaji ya juu ya umeme nchini yamefikia Megawatts 1,273 hadi kufikia Oktoba mwaka huu na kwamba uwezo wa mitambo ya kufua umeme uliounngwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa umefikia Megawatts 1,573 ambapo umeme wa nguvu ya maji ni asilimia 36.46 ,gesi asilimia 57.28 ,mafuta asilimia 5.60 na tungamotaka asilimia 0.67.
Ametaja mafanikio mengine katika sekta hiyo kuwa ni kukamilika kwa mitambo ya kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji,kukamilika kwa ujenzi wa mitambo ya kufua umeme kwa kutumia gesi asilia,kukamilika kwa kwa ujenzi wa njia za kusafirisha umeme ,kuendelea na utekelezaji wa mpango Kabambe wa kusambaza umeme vijijini wa REA I,REA II na REA III).
"Miradi hiyo ya REA imewezesha vijiji 10,361 kupatiwa umeme,hadi kufikia Juni mwaka huu sawa na asilimia 86 ya vijijini vyote 12,268,kuendelea kuunganisha umeme wateja wapya nchini kwa kasi,"amesema.
Mhandisi Mramba amesema, mafanikio mengine ni kukamilika kwa ujenzi wa vituo vipya vya kupoza umeme kwa ajili ya kuboresha upatikanaji umeme,kukamilika kwa ujenzi wa vituo vipya vya kupoza umeme,kukamilika kwa ujenzi wa njia za umeme,kukamilika kwa mradi wa kusambaza umeme,kujengwa na kukamilika kwa 'submarine cable' mbili zilizopo chini ya bahari,kukamilika kwa mradi wa ORIO na kukamilika kwa sera,sheria na kanuni zinazosimamia Sekta ya Nishati.
Pia kukamilika kwa kanuni mbalimbali kwa ajili ya udhibiti huduma za nishati, kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji umeme nchini,kuongezeka kwa idadi ya taasisi zilizopatiwa umeme vijijini ,kuandaliwa na kuanzia kutumika kwa mikataba mahsusi ya kuuziana umeme,kukamilika kwa mradi wa kuboresha mfumo wa usambazaji umeme katika jiji la Dar es Salaam na kukamilika kwa utekelezaji wa Program ya Awamu ya Pili ya Mradi wa Sustainable Solar Market Package (SSMP-II) wa 2016.
Pia amesema, mafanikio mengine ni kuunganishwa kwa mikoa katika Gridi ya Taifa isipokuwa mikoa minne ya Kigoma,Katavi,Kagera na Rukwa,kusitisha matumizi ya mitambo ya kukodi ya binafsi ya kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta mazito,kusitisha uingizaji wa vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya umeme ikiwemo nguzo,transfoma,nyaya na mita za luku,kugundulikwa kwa maeneo yanayoweza kuzalisha umeme kutokana na joto ardhi na kuwezesha matumizi ya umeme jua katika maeneo ya huduma za kijamii.
Mhandisi Mramba amesema, mafanikio yote hayo yamewezesha upatikanaji na uzalishaji umeme nchi nzima tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya Uhuru huku akisema hayo ni mafanikio makubwa kwani imepelekea ukuaji wa uchumi hadi kufikia uchumi wa kati.
Kwani upande wa mafanikio ya mafuta na gesi Mramba amesema, baadhi ya mafanikio ni kugundulika kwa gesi asilia katika maeneo ya Songosongo, Mnazi bay,Mkuranga, Kilwa Kaskazini na kina kitefu cha bahari ambapo gesi iliyogunduliwa nchi kavu na kina kirefu cha bahari ni futi za ujazo trilioni 57.54 mwaka 2021.
Mhandisi Mramba amesema, ugunduzi huo umewezesha kuanza kutumika kwa gesi asilia kama chanzo cha nishati hususani kwa kuzalisha umeme viwandani,majumbani na kwenye magari ambapo hadi kufikia Oktoba mwaka huu viwanda 52 jijini Dar es Salaam, Pwani na Mtwara vinatumia gesi asilia.
Amesema,matumizi ya gesi asilia yamesaidia kupunguza utegemezi wa uzalishaji umeme kwa kutumia nguvu za maji ambapo hadi Novemba, 2021 takribani asilimia 60 ya umeme nchini inazalishwa kwa kutumia gesi asilia.
"Katika kipindi cha mwaka 2004 hadi Juni 2020 matumizi ya gesi asilia ya Mnazi bay na Songosongo yamesaidia serikali kuokoa shilingi trilioni 38 ambazo zingetumika kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya mitambo ya umeme na viwandani ambapo hadi sasa mapato yanayotokana na mauzo ya gesi yamechangia zaidi ya shilingi bilioni 208 katika mfuko wa mafuta na gesi kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 baada ya kukamilika ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara/Songosongo hadi Dar es salaam,"amesema Mhandisi Mramba.
Pia amesema hadi Disemba 2020 Serikali imepata mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 441 yanayotokana na kodi mbalimbali kuanzia mwaka 2015 baada ya kukamilika kwa mradi wa Bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara/Songosongo hadi Dar es salaam.
Mheshimiwa Mhandisi Mramba ameyataja mafanikio mengine yaliyopatikana katika mafuta na gesi asilia kuwa ni Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kulipa zaidi ya shilingi bilioni 10 katika mwaka 2018/19 na mwaka 2019/2020 ikiwa ni gawio kwa serikali.
Aidha, amesema hadi Juni magari 750 yamewekwa mfumo wa matumizi ya nishati ya gesi asilia pamoja na kuanzishwa na kuendelea kuimarika kwa mfumo wa uigizaji wa mafuta kwa pamoja ambao umeongeza uhakika wa upatikanaji wa mafuta nchini na kupunguza gharama za uagizaji wa nishati hiyo.