NA MWANDISHI MAALUM
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu ndani ya kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara imepata mafanikio mengi.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuboresha mfumo wa kielektroniki wa kushughulikia maombi ya vibali vya kazi kwa raia wa kigeni ikiwa ni pamoja na kusimamia, kuboresha na kusanifu mfumo wa vibali nchini.
Mheshimiwa Mhagama ameyasema hayo Novemba 23, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya ofisi yake katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Amesema kuwa, mfumo huo umepunguza muda wa kushughulikia maombi ya kibali kutoka siku za kazi 14 zilizopo kisheria hadi siku saba kutokana na kupungua kwa hatua za uombaji wa kibali kutoka hatua 33 hadi hatua tatu pekee.
“Aidha mfumo huu umeunganishwa na mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala ya Usajili wa biashara na leseni (BRELA) na inategemewa Taasisi nyingi zaidi za serikali zitaendelea kuunganishwa na mfumo huu,”amesema Waziri Mhagama.
Mheshimiwa Mhagama, pia amesema kuwa, mafunzo kuhusu utumiaji wa mfumo yametolewa kwa watendaji wa ndani na nje ya Serikali.
Amefafanua kuwa, hata mfumo huo umeimarisha uwazi na uwajibikaji, kupunguza urasimu na vihatarishi vya rushwa katika kushughulikia vibali.
MAFAO YA WATUMISHI
Waziri Mhagama amesema kuwa, ndani ya kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara ofisi yake inakamilisha utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kuimarisha mfumo wa mafao ya watumishi kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Amesema, anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuangalia utaratibu wa kulipa madeni ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
“Naishukuru Serikali ya Mama Samia inaendelea kuangalia madeni haya yote na kuona utaratibu wa kulipa na inafanya utaratibu wa kulipa shilingi trilioni 4.6.Tunaamini kwa mwenendo huu kwa 'commitment' ya Serikali tunapoenda madeni yataisha na utatengenezwa mfumo bora,”amesema.
Waziri Mhagama amesema, kwa sasa Ofisi ya Waziri Mkuu inakamilisha utekelezaji maelekezo ya Serikali ya kuimarisha Mfumo wa Mafao ya watumishi kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
PSSSF KIGANJANI
Waziri Mhagama amesema, mfumo wa Kielektroniki wa PSSSF Kinganjani una maeneo mawili, eneo la wanachama na eneo la waajiria ambapo amedai mfumo huo unatoa fursa kwa mwanachama ya kupata taarifa ya mwajiri kuhusu mawasilisho ya michango ya wanachama, usajili na madeni ya michango yake ambayo haijalipwa.
Pia unarahisisha upatikanaji wa taarifa za michango ya wanachama, unarahisisha ufuatiliaji wa malipo ya Pensheni ya kila mwezi kwa mwanachama.
Amesema, tangu Tanzania Bara ipate uhuru, sekta ya hifadhi ya jamii imepitia mabadiliko chanya yaliyolenga kuboresha huduma za Hifadhi za Jamii kwa Wananchi wa Tanzania.
Amesema, mwaka 1962, Serikali ilipanua wigo wa watumishi wanaohudumiwa na Mfumo wa Pensheni kwa kuwajumuisha Waalimu wazalendo kwani kabla ya hapo Mfumo ulikuwa unahudumia watumishi wa Serikali Kuu pekee.
Amesema, mwaka 1964 ulianzishwa Mfuko wa Akiba kwa watumishi kwa Sekta Binafsi (NPF) baadaye mwaka 1998 ulianzishwa Mfuko wa NSSF ambao unahudumia watumishi wa Sekta Binafsi.
Hata hivyo, mifuko ya GEPF (1942), LAPF (1944) iliyokuwa imeanzishwa kabla ya Uhuru ambayo ilihusisha Wafanyakazi wa Serikali kuu waliokuwa wa Mikataba (Non Pensionable) na Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa.
Waziri huyo amesema Mwaka 2010, 2014 na 2018 Serikali iIifanya mabadiriko makubwa ya kuboresha Sekta ya Hifadhi ya jamii kwa Serikali ilianzisha Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii.
Pia,Mwaka 2014 Serikali ilifanya mabadiliko ya Sheria ya SSRA ili kuwianisha mafao kwa watumishi wanaostaafu katika sekta ya Umma na Binafsi.
Amesema Mwaka 2008, Serikali ilitunga Sheria mpya na kuanzisha Mfuko wa Fidia kwa Wafanya Kazi (WCF) ambao ulianzishwa rasmi mwaka 2015 ili kuondokana na Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi ya Mwaka 1957 na Mapitio yake ya mwaka 2002 ambayo haikuwa inatenda haki katika kuoanisha viwango vya malipo ya fidia kwa ulemavu na madhara yatokanayo na kazi.
Amesema Mwaka 2018 Serikali iliunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii minne ya GEPF, LAPF, PSPF na PPF kuwa mfuko mmoja wa PSSSF wa watumishi wa Umma.
VYAMA VINGI
Waziri huyo amesema Mfumo wa Demokrasia ya vyama vingi vya Siasa ulikuwapo kabla ya uhuru na mara baada ya uhuru.
“Kati ya mwaka 1965 mpaka 1992 tulikuwa na mfumo wa chama kimoja. Mwaka 1992 Nchi yetu ilirejesha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya Siasa ili kupamua wigo wa demokrasia,”amesema.
Amesema Mwaka 1992, Sheria ya Vyama vya Siasa na. 5 ilitungwa na kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.
“Vyama vya Siasa vilianza kusajiliwa tena mwaka 1992 ambapo katika Uchaguzi Mkuu wa vyama vingi vya Siasa mwaka 1995 vyama vya Siasa 13 vyenye usajili kamili viliweka wagombea.
“Toka mwaka 1992 mpaka sasa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imekwisha toa vyeti vya usajili wa muda kwa vyama vya Siasa 81 na imetoa vyeti vya usajili kamili kwa vyama vya Siasa 25 na kufuta usajili wa vyama vya Siasa vyenye usajili kamili 6 ambavyo vilikiuka masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa,”amesema.
Amesema, hivi sasa kuna vyama vya siasa vyenye usajili kamili 19 na Chama kimoja cha siasa chenye usajili wa muda.
Aidha, Sheria ya vyama vya Siasa imekuwa ikiboreshwa mara kwa mara ili kuendana na mahitaji ya wakati husika na kuiwezesha kukabili changamoto zilizopo na zitakazojitokeza.
TUME HURU YA UCHAGUZI
Waziri Mhagama amesema mafanikio ambayo imeyapata ndani ya miaka 60 ya uhuru ni kuwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo ni huru na inafanya kazi kwa mujibu wa sheria na wala Serikali haiingilii majukumu yake.
Waziri huyo amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilianzishwa Januari, 14 mwaka 1993 chini ya Ibara ya 74(i) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
Aidha, Ibara ya 74 (7) na (11) inaeleza kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni Huru na katika utekelezaji wa majukumu yake haipokei amri au maelekezo kutoka kwa mtu au Taasisi yoyote.
Amesema lengo kuu la kuanzishwa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni kuendesha, kusimamia na kuratibu Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani chini ya Mfumo wa Siasa wa Vyama Vingi.
Amesema Majukumu mengine ya Tume ni pamoja na Kusimamia na kuratibu Uandikishaji wa Wapiga Kura katika Uchaguzi wa Rais na Wabunge katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania Bara; Kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Majimbo ya Uchaguzi wa Wabunge na Kutoa Elimu ya Mpiga Kura Nchini kote.
Amesema Mpaka sasa Tume ya Uchaguzi imefanikiwa kusimamia Chaguzi Kuu 6 za mwaka 1995, 2000, 2005, 2010,2015, 2020.