Miaka 60 ya Uhuru:Tembea kifua mbele, Tanzania ni salama saa 24

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt.Stargomena Tax amesema katika miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeendelea kulinda mipaka ya nchi na inaendelea kuwa salama saa 24.
Pia amesema wizara hiyo kupitia JWTZ lipo tayari muda wowote na limejipanga kuhakikisha wanayadhibiti matukio ya kigaidi kabla hayajatokea kwa kushirikiana kwa karibu na nchi za Umoja wa Afrika.

“Kwa ujumla hali ya mipaka baina ya nchi yetu nan chi jirani imeendelea kuwa salama,"amesema Dkt.Tax.

Aidha, amesema,dira ya wizara hiyo ni kuifanya Tanzania yenye amani huku dhima ikiwa ni kulinda mamlaka,mipaka ya nchi na maslahi ya Taifa.

Mheshimiwa Dkt.Tax ameyasema hayo Novemba 29, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Dkt.Tax amesema, kazi hiyo inafanywa kwa kutekeleza sera ya ulinzi wa Taifa katika kudumisha amani na usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tunapoelekea katika maadhimisho ya miaka 60 baada ya Uhuru wa Tanzania Bara,Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa linaendelea na majukumu yake huku dhima kubwa ikiwa ni kulinda mamlaka ya nchi na maslahi ya Taifa,"amesema Dkt.Tax.

Aidha, amesema majukumu ya wizara hiyo ni kuliongezea uwezo wa kimedani Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kulipatia vifaa na zana bora pamoja na mafunzo na mazoezi.

Vile vile,kuboresha mazingira ya kufanyia kazi,makazi na kuimarisha upatikanaji wa huduma stahiki na mahitaji ya msingi kwa wanajeshi na watumishi wa umma na kuwapa vijana wa kitanzania mafunzo ya awali ya kijeshi na stadi za kazi ili kuwajengea ukakamavu,uzalendo umoja wa kitaifa na uwezo wa kujitegemea.

Pia amesema majukumu mengine ni kuendelea tafiti za kiuhawilishaji kwa ajili ya kuzalisha bidhaa na huduma kwa matumizi ya kijeshi na raia pamoja na kutoa mafunzo ya jeshi la akiba katika mikoa yote na kuimarisha Ushirikiano nan chi nyingine katika Nyanja za kijeshi na kiulinzi.

MAFANIKIO
Mheshimiwa Dkt.Tax akizungumzia kuhusu mafanikio ya Serikali kupitia wizara hiyo amesema ,tangu nchi ipate Uhuru Jeshi la Wananchi wa Tanzania limefanya mageuzi na kupata mafanikio makubwa huku mipango ya baadaye ya jeshi hilo ni kuwa na jeshi dogo lenye wataalam,zana na vifaa vya kisasa.

Aidha,wizara hiyo kupitia JWTZ imeendelea kutoa nafasi ,mafunzo mbalimbali ya kozi za kijeshi katika shule na vyuo vya kijeshi ndani na nje ya nchi lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kiutendaji kivita maafisa na askari katika kutekeleza majukumu yao ya msingi ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Dkt.Tax pia wizara kupitia JWTZ imeendelea kuimarisha shule na vyuo vya kijeshi vya maafisa na askari katika kuboresha mafunzo.

Akizungumzia kuhusu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa vijana ambapo alisema,tangu kuanzishwa kwa JKT imeendelea kutekeleza mafunzo ya vijana kwa ufanisi hadi mwaka 1994 yalipositishwa kutokana na kuyumba kwa kwa uchumi wa dunia miaka ya 1980 hadi 1990.

Alisema, mafunzo hayo yalirejeshwa mwaka 2001 kwa vijana wa kujitolea na mwaka 2013 kwa vijana wa mujibu wa sheria huku akisema mafunzo hayo yamekuwa na mafanikio makubwa kwa Taifa yakijumuisha kuongezeka kwa ualendo kwa vijana waliopitia mafunzo ya JKT na hivyo kupunguza adha mbalimbali ikiwemo migomo kwa vyuo vikuu.

Vile vile alisema wizara hiyo kupitia JKT imeendelea kutekeleza mkakati wa kilimo 2019/2020-2024/25 ambao umelenga kuliwezesha JKT kujitosheleza kwa chakula .

Mkakati huo unatekelezwa katika vikosi vya Chita-Morogori,Milundikwa –Rukwa, Mlale-Ruvuma, Mgambo-Tanga na Oljoro Arusha mkakati ambao unatekelezwa kupitia vyanzo vya ndani vya mapato vya JKT na bajeti ya Serikali.

Pia amesema,wizara hiyo kupitia JKT inashiriki katika kilimo cha mazo ya kimkakati ya Taifa ambayo ni michikichi Bulombora-Kigoma,Mkonge Mgambo na Malamba –Tanga,korosho Nachingwea Lindi na Manyoni mkoani Singida ,alizeti –Makutupora Dodoma na Kahawa –Itenda Mbeya na Tarime-Mara.

Amesema,katika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi wizara kupitia JKT inaendelea na ujenzi wa mfumo wa umwagiliaji katika shamba la mpunga –Chita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news