NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Mheshimiwa Siriel Mchembe ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga ameagiza Jeshi la polisi wilayani humo kumkamata na kumhoji Afisa Tarafa ya Mazingara, Amin Yasin.
Afisa tarafa huyo anatuhumiwa kuomba rushwa ya shilingi milioni nne ili kuwaruhusu watu kuishi katika msitu wa Mkulumilo wilayani humo.
Aidha, Mheshimiwa Mchembe amemsimamisha kazi afisa huyo kwa siku saba ili kupisha uchunguzi juu ya tuhuma hizo.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, afisa huyo amesababisha kutokea sitofahamu kwa wananchi kuandamana wakimtafuta mkuu wa wilaya ili kuweza kutatua kero hiyo.
Akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Amani, Novemba 6,2021 baada ya kusikiliza pande zote DC Mchembe ametoa maagizo kwa jeshi la polisi kumkata afisa huyo na kumhoji.
Mchembe amesema, hawezi kumfukuza mtumishi huyo kazi kwa kuwa ameajiriwa na mamlaka nyingine, ila kutokana na maelezo ya wananchi na viongozi wengine afisa huyo akahojiwe Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
"Maagizo yangu OCD mchukue huyu afisa Tarafa nendeni mkaongee nae kwamba suala hili lilikuwaje na muafaka nini, mkipata taarifa basi mnishauri nini cha kufanya juu yake. Ila kwa mamlaka niliyonayo nina msimamisha kazi kwa siku saba ili kupisha uchunguzi dhidi yake juu ya tuhuma za rushwa na matumizi mabaya ya madaraka," amesema Mchembe.
Mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Guse amesema mbele ya mkuu huyo wa wilaya kuwa, walitakiwa kuhama katika Kijiji cha Mkulumilo ambacho kipo ndani ya hifadhi ila wakati mchakato unaendelea afisa tarafa aliitisha kikao na baadae kuwaomba wananchi shilingi milioni nne ili aweze kufanya utaratibu wabaki katika eneo hilo.
"Nilimrekodi tukiwa tunaongea kwenye simu kwamba tufanye mpango ili tusifukuzwe ndani ya eneo tuchangishane kiasi hicho cha fedha tumpatie na yeye kuna wenzake atawapatia ili tuweze kuachwa kwenye hifadhi,mkuu wa wilaya sisi tumechoka kufanywa ATM na hawa viongozi tunataka suluhisho," amesema Guse.
Kwa upande wake, Theresia Simoni ameongeza kuwa licha ya afisa tarafa huyo kutuhumiwa kuomba rushwa pia wanamtuhumu kwa kuwaondoa wenyeviti wa vijiji wanaowachagua na badala yake kuweka wa kwake bila kuwashirikisha viongozi wenzake na wananchi.
Naye afisa tarafa anayetuhumiwa kukusanya fedha hizo, Amin Yasini amesema alizikusanya kwa ajili ya kuwajadili wananchi waliovamia kwenye msitu huo na baadae wajumbe walikataa na akazirudisha kwa wahusika.
"Baada ya kupokea zile shilingi milioni nne nilianza kuangalia uhalali wa ule msitu wa hifadhi na baadae nikagundua kuwa hapaswi mtu kuishi mule na wale wapo kimakosa,hivyo nikaamua kuzirudisha baada ya kugundua zinaweza kunitokea puani,"amesema Yasin.
Aaidha, afisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Patrick Katemba amesema suala hilo lina viashiria vya kushawishi utoaji na upokeaji rushwa.
Katemba amesema kutokana na viashiria hivyo, ofisi yake itafuatilia ili kuona kuna makosa au hapana kwenye mchakato wa ukusanyaji fedha hizo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Handeni, Athumani Malunda amesema afisa huyo ana matukio mengine kama hayo, hivyo kumuomba Mkuu wa wilaya kuangalia ni jinsi gani watatumia utaratibu wa kuweza kukomesha masuala hayo ili yasiweze kutokea tena.