NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuzindua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Wakulima Tanganyika (TFA) utakaofanyika leo Novemba 6,2021 katika Chuo cha Uhasibu jijini Mbeya.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Mwingulu Nchemba. (NA MAKTABA).
Mkurugenzi Mtendaji wa TFA, Justine Shirima amesema kuwa, chama katika juhudi zake za makusudi za kuwahudumia Wananchi na Wakulima nchini, kimeandaa mkutano huo mahasusi kwa wakulima na wanahisa wake kote nchini.
Shirima amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kuzileta pamoja kampuni za kimataifa ambazo zina uzoefu wa muda mrefu katika kuwahudumia wakulima kwa utaalamu wa hali ya juu ili kuzalisha mazao bora.
Amesema kuwa,” mkutano huu utajumuisha makampuni na washirika kutoka Marekani, Brazili, India, China na Ulaya ambazo zitasaidia kuleta uzoefu wa kitaalamu ambao utakuwa na tija kwa wakulima wa Tanzania.
Aidha, Mkurugenzi huyo amesema kuwa mkutano huo pia utaleta mapinduzi makubwa ya kilimo katika usimamizi wa mbolea na udongo ambao kwa hakika utaongeza mavuno na mapato ya wakulima.
”Yote haya yataongeza ujuzi na uzoefu ambao jumuiya ya wakulima Tanzania na Afrika inakosa na hivyo tunatarajia kujenga ushirikiano imara kwa maendeleo ya Kilimo chetu cha Tanzania.
”Ili kuhakikisha haya yote yanatokea tuna washirika kutoka pande zote za dunia ambao wanatuunga mkono ili kufikia malengo haya makubwa,” amesema Shirima.
Katika mkutano huu pia TFA itatambulisha bidhaa mpya ya mbolea ‘TFA FAHARI’ ambayo ni bolea bora na halisi lakini pia inakidhi vyema hali ya udongo kwenye mashamba mengi nchini.
Hivi karibuni TFA ilizindua mpango wa kuchambua viwango vya udongo yaani ‘soil PH’ ili kuwawezesha wakulima kupunguza matumizi ya mbolea ya viwandani na kuchochea mbolea bora na halisi.
KUHUSU TFA
TFA ni mmoja wa wadau wakubwa na wenye ufanisi zaidi katika sekta ya kilimo nchini Tanzania tangu ilipoanza shughuli zake Tanganyika, mwaka 1935.
Chama hicho kina wanachama zaidi ya 4,800 wanaowakilisha sehemu mbalimbali za Jumuiya ya wakulima wa Tanzania ikiwa ni sambamba na mtandao wa usambazaji wa matawi zaidi ya 17 nchini.