NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Regina Kihwele maarufu kama Gynah ambaye amebobea katika fani ya muziki, uandishi, uigizaji na uanamitindo ameibuka mshindi katika uigizaji bora wa kike kwenye tuzo za Lake International Pan African Film Festival (LIPFF).
Ni kupitia hafla iliyofanyika Novemba 6, 2021 nchini Kenya na kuwabwaga waigizaji wengine kutoka Jamhuri ya Afrika Kusini,Cameroon, Morocco na Uganda.
Gynah baada ya kupokea tuzo hiyo amesema, anamshukuru Mungu kwa kumuwezesha kufikia hatua hiyo muhimu na anaamini ataendelea kumuwezesha kufanya makubwa zaidi siku zijazo.
Amesema, tuzo za LIPFF zimeandaliwa na Legacy Arts ambapo washiriki wa tuzo hizo zilikuwa nchi tano ikiwemo kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Cameroon,Afrika ya Kusini,Morocco na Uganda.
Gynah amesema, tuzo aliyoshinda katika FILAMU YA MULASI ambayo imebeba jina linalotokana na lugha ya Kabila la Wagogo inamuangazia mwanamke aitwaye Sechelela ambaye ana usongo wa mawazo na anapitia kipindi kigumu kati yake na familia yake ikiwemo kazi zake.
Amesema, filamu hiyo imeongozwa na Honeymoon Aljabri mwenye tuzo za utengenezaji na uongozaji filamu, aliyezaliwa na kukulia jijini Dodoma, lakini makao yake yapo nchini Marekani.
"Nimeigiza kama muigizaji mkuu Sechelela,Sechelela ni mwanamke jasiri anayebeba machungu mengi ambayo wanawake wengi wakitanzania kwenye ndoa zao huficha. Tuzo hizi zimekuwa daraja la kukuza sekta ya filamu na utalii wa Tanzania kupitia waigizaji wadogo wadogo wa kike walioshinda tuzo hizo,"amesema.
Gynah ametoa wito kwa vijana chipukizi hususani wasanii kushiriki katika filamu za kuonyesha tamaduni zetu za kiafrika na kupenda wanachokifanya huku wakiwa wavumilivu na wakipata nafasi wajitume na kufanya kazi kwa bidii kwani watapata mafanikio makubwa.