NA MWANDISHI DIRAMAKINI
BARAZA la Madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora limeazimia kufukuzwa kazi Mtumishi wa Idara ya Maabara katika Kituo cha Afya Mazinge Godfrey Mwanyika kwa tuhuma za kuiba kifaa cha hospitali (darubini).
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Rashid Maulid Magope (aliyekaa katikati mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa halmashauri hiyo baada ya kumalizika mafunzo kwa madiwani na watumishi wa halmashauri hiyo.(Picha na MWANDISHI DIRAMAKINI).
Akitoa taarifa ya maazimio hayo yaliyofikiwa baada ya baraza kukaa kama Kamati ya Nidhamu, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Rashid Magope amesema wamefikia uamuzi huo baada ya mtumishi huyo kukiuka maadili ya utumishi wa umma.
Magope amesema, mtumishi huyo alikamatwa na kifaa hicho maeneo ya nyumbani kwake wilayani humo huku akijua kuwa kumiliki mali ya halmashauri kinyume na utaratibu ni kosa la jinai, tume iliundwa na kuchunguza suala hilo na mtuhumiwa akafikishwa mahakamani.
Alibainisha kuwa mahakama ilimwachilia huru baada kukosekana ushahidi wa kutosha, ila baada ya kurejea suala lake lilirudishwa kwenye Mamlaka ya Nidhamu kutokana na mwenendo wake unaotia shaka ikiwemo kuwahi kutuhumiwa kutoboa dari ya ofisi ili kuingia chumba chenye dawa kwa nia ya kuiba.
Mwenyekiti amefafanua kuwa, licha ya mtuhumiwa huyo kusamehewa katika tukio hilo la kujaribu kuiba dawa, uadilifu wake kama mtumishi wa umma unatia shaka ndiyo maana alisimamishwa kazi, na sasa wameazimia afukuzwe moja kwa moja.
"Tumeazimia kufukuzwa kazi Mtaalamu wetu wa Maabara aliyekuwa katika Kituo cha Afya Mazinge kutokana na kukabiliwa na tuhuma mbalimbali ambazo ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma,"amesema.
Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mayeka Tungu amesema kuwa, hakuna diwani anayependa mtumishi yeyote wa halmashauri kufukuzwa kazi ila inapobainisha tabia na mwenendo wa mtumishi fulani hauridhi watachukua hatua.
Amesisitiza kuwa baraza halipo kwa ajili ya kumwonea mtu au kufukuza mtumishi ila kila Mtaalamu anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia maadili na taratibu za utumishi wa umma na sio kufanya ujanja ujanja ili kujinufaisha.
Pia amewataka watumishi wa umma wote waliopewa dhamana ya kusimamia utoaji huduma kwa jamii kutekeleza shughuli zao kwa uadilifu mkubwa na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kudhalilisha taaluma zao.
Alipotafutwa Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu wa halmashauri hiyo, Nico Kayange ili kulitolea ufafanuzi wa kina suala hilo alisema kuwa atatoa taarifa rasmi juu ya suala hilo na hatua zilizochukuliwa hivi karibuni.