NA GODFREY NNKO
"Kitambo kidogo tu nikiisha kuwaondokea, nikamuona mpendwa wa nafsi yangu, nikamshika, nisimuache tena, hata nilipomleta nyumbani mwa mama yangu, chumbani mwake aliyenizaa;
Ujumbe huo wa neno la Mungu kutoka katika kitabu cha Biblia Takatifu katika Wimbo Ulio Bora wa Sulemani 3:4 umesindikiza tabasamu la wawili wapendanao ambao ni Mwinjilisti na Nabii wa Kimataifa kutoka nchini Kenya, Dkt.Lucy Natasha na mpendwa wake aliyemtambulisha kwa jina la Carmel.
Dkt.Lucy Natasha ametoa mstari huo katika Biblia huku ukisindikizwa na ujumbe wa, "Nimempata yule ambaye nafsi yangu inampenda" kulingana na Wimbo Ulio Bora wa Suleimani 3.4 huku ukisindikizwa na picha mfululizo.
Wawili hao wametoa majibu rasmi ya ukimya wa Mwinjilisti huyo ambaye mara nyingi alionekana kuwa hana mume huku maswali mbalimbali yakielekezwa kwake na wafuasi wake katika mitandao ya kijamii na hata nje na ndani ya huduma bila majibu.
Dkt.Lucy na Carmel wakiwa wamevalia mavazi ya kupendeza na ya kufanana ya jamii ya Wahindi, yanayojulikana kama 'sarees', mwana dada huyo mrembo na mtumishi wa Mungu ameonekana akiwa na furaha huku aliyempata akimtengenezea vazi lake.
Wakati akimtengenezea, kwa upande wa Carmel, alionekana kuonyesha unyenyekevu wa hali ya juu kwa kupiga magoti ikiwa ni moja wapo ya ishara ya unyenyekevu na upendo.
Mwasisi huyo wa huduma mbalimbali ikiwemo Empowerment Christian Church Nairobi, ni miongoni mwa watu mashuhuri zaidi ndani na nje ya Kenya, kwani kupitia huduma zake anazofanya amekuwa akizifanya kama semina katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Ulaya, Mashariki ya Mbali, Bara la Afrika na kwingineko.
Dkt.Natasha anafundisha Biblia na anafundisha elimu ya maisha hivyo amekuwa akiwagusa wengi ndani na nje ya Kenya.
"Tunawathamini sana watoto wetu wa kiume, mabinti, washirika wa Kimataifa, ECC Duniani kote, marafiki na familia kwa usaidizi wenu. Upendo wangu na Carmel utawezesha safari yetu yote ya maisha pamoja ijazwe kwa neema, baraka, riziki, ulinzi na mwongozo wa Mungu. Tutaendelea kumtumikia Mungu na kuwabariki wanadamu. Tukutane ECC Nairobi kwa IBADA YETU YA KUSHEREHEKEA Jumapili hii (Novemba 28, 2021) saa 10.00 asubuhi,"ameeleza Dkt.Lucy Natasha katika ukurasa wake wa Facebook huku akiambatanisha na picha wakiwa wamevalia rasmi mavazi ya harusi.