NA ROTARY HAULE
NAIBU Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Ajira na Walemavu, Ummy Ndeliananga amewataka walemavu hususani wasioona kuhakikisha wanajitokeza kushiriki zoezi la Sensa linalotarajiwa kufanyika Agosti 2022.
Ndeliananga ametoa wito huo leo Novemba 4 katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Fimbo Nyeupe yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya stendi ya zamani Mailimoja vilivyopo Kibaha mkoani hapa.
Alisema kuwa, Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuratibu na kuweka sawa mipango ya kisheria,kanuni na taratibu za watu wenye ulemavu katika kutetea haki zao na kutoa huduma za msingi.
Alisema kuwa, kutokana na hali hiyo ni lazima walemavu wote kupitia vyama vyao wakawa mstari wa mbele kujitokeza kuhesabiwa katika Sensa ya mwaka 2022 ili kuisaidia Serikali katika kuwafikia Walemavu wote waliopo nchini.
"Ndugu zangu tunapoadhimisha Leo siku ya Fimbo Nyeupe ni lazima pia tukumbuke suala la Sensa lililopo mbele yetu na mimi Waziri wenu nachukua fursa hii kuwaomba wenzangu twende tukahamasishane kushiriki Sensa hiyo kwa faida yetu na faida ya Taifa letu,"alisema Waziri Ndeliananga
Aidha,mbali na Sensa lakini pia Ndeliananga amewakumbusha watu wote wenye ulemavu nchini kuhakikisha wanajitokeza kuchanja chanjo ya UVIKO-19 kwa ajili ya kujilinda wao wenyewe na familia zao.
Alisema,Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan,amefanyakazi kubwa kwa ajili ya kutaka kuwakomboa watu wake juu ya ugonjwa huo ndio maana amefanikiwa kuleta chanjo hiyo kwahiyo ni vyema tukaunga mkono juhudi hizo.
"Ndugu zangu Walemavu nawaomba Sana mjitokeze kuchanja chanjo ya UVIKO-19 kwa faida yetu,chanjo hiyo ni salama na wala haina madhara yoyote na hata mimi mwenyewe nimechanja siku nyingi na mpaka leo nipo mzima sijapatwa na madhara yoyote,", alisema
Aliongeza kuwa,kamwe wasikae na kusikiliza maneno ya watu wapotoshaji kwakuwa watu wa aina hiyo hawana nia njema na Watanzania lakini kinachotakiwa ni kuchanja ili kujilinda dhidi ya ugonjwa huo.
Akizungumzia kuhusu elimu kwa watoto wenye ulemavu Waziri Ndeliananga alisema Serikali inaendelea na utaratibu wa kujenga miundombinu ya shule za Walemavu nchini.
Alisema kwasasa tayari Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kujenga Shule za Sekondari kwa ajili ya walemavu pamoja na mabweni yake ikiwa na lengo la kuhakikisha Walemavu Wasioona na wengine wanapata elimu sawa na jamii nyingine ya kawaida.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Cha Watu Wasioona Tanzania (TLB)Omary Mponela ,aliishukuru Serikali kwa namna inavyojitoa kusaidia Walemavu katika sekta mbalimbali.
Mponela,alisema kuwa miongoni mwa mambo magumu ya kujivunia ni pamoja na kutoa usawa wa kielimu kwa kujenga miundombinu mbalimbali ya Shule ,kutoa misaada ya vifaa pamoja na mikopo kwa wajasiriamali Walemavu.
"Mheshimiwa Naibu Waziri sisi leo tupo hapa lakini tunafarijika sana na Serikali yetu kwakuwa inatusaidia katika mambo mengi na tunaomba iendelee hivyo ili na sisi tupate yale mahitaji muhimu ya kila siku Kama wengine,"alisema Mponela
Mponela,aliomba Serikali kuhakikisha inatoa ruzuku kwa vyama vya watu wenye ulemavu ili viweze kujiendesha kuliko kutegemea wafadhili pekee ambao wakati mwingine wanakwama kutekeleza mahitaji yao.
Hatahivyo,Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sarah Msafiri, alisema kuwa anaendelea kushirikiana na Walemavu katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo hususani katika kuweka misingi yao imara.
Tags
Habari