Nane wavuliwa uchungaji, wasimamishwa kazi KKKT

NA GODFREY NNKO

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Mashariki limewasimamisha kazi watumishi wake nane.

Hayo yamebainishwa kupitia barua yenye kumbukumbu namba NED/EC/Vol/11/021 iliyoonwa na DIRAMAKINI BLOG ambayo imesainiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mchungaji Godfrey T.Walalaze.

Kwa mujibu wa barua hiyo ambayo nakala yake imetumwa kwa viongozi mbalimbali imeelezea kuwa, uamuzi huo umefikiwa baada ya kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya KKKT (DKMs) kilichokaa Oktoba 29, 2021 huko Utondolo mjini Lushoto.

"Ninasikitika kuwajulisha kuwa, katika kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya KKKT-DKMs, kilichokaa tarehe 29, 10, 2021 Utondolo Lushoto, kilipitia kwa kina taarifa ya ukaguzi wa hesabu kwa kipindi cha 2019 na 2020.

"Baada ya mapitio hayo na kutafakari kwa umakini mkubwa, Halmashauri Kuu ilifikia uamuzi wa kuwavua uchungaji na kuwasimamisha kazi watumishi kutokana na sababu zifuatazo.

"Kushindwa kusimamia mali za dayosisi wakati wa uongozi wao, kutumia vibaya madaraka yao kulikosababisha uvunjwaji wa Katiba ya KKKT-DKMS, kufanya mambo yanayosababisha migongano na hivyo kuchochea vurugu na ukosefu wa amani miongoni mwa waumini, watumishi na dayosisi kwa ujumla.
"Kwa kuzingatia sababu hizo hapo, halmashauri iliamua ifuatavyo, mosi Dkt.Stephen Ismail Munga, aliyekuwa Askofu wa Dayosisi na Mdhamini wa mali avuliwe uchungaji na hivyo kupoteza sifa ya kuwa askofu mstaafu wa DKMs, pili mchungaji Dkt.Eberhadt S.Ngugi ambaye alikuwa msaidizi wa Askofu na Mdhamini wa mali amesimamishwa uchungaji.

"Tatu, mchungaji James E.Mwinuka, aliyekuwa Katibu Mkuu na Mdhamini wa mali amesimamishwa uchungaji, nne mchungaji Dkt.Anneth Munga aliyekuwa Katibu Mkuu na Mdhamini wa mali amesimamishwa uchungaji, tano mchungaji Yambazi T.Mauya aliyekuwa Mkuu wa Jimbo (Dinari) la Tambarare amesimamishwa uchungaji, sita mchungaji Paulo Diu aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Kikristo na Elimu amesimamishwa uchungaji, saba mchungaji Yohana Titu aliyekuwa Chaplain wa Hospitali ya Bombo amesimamishwa uchungaji na mwisho ambayo ni namba nane ni Bw.Rodgers Sgehumu aliyekuwa mtunza hazina wa Jimbo la Tambarare na Hospitali ya Lutindi amesimamishwa kazi,"amefafanua kwa kina Kaimu Katibu Mkuu huyo.

Hata hivyo, ametoa wito kwa waumini kuzidi kuombea utulivu, amani na umoja wadayosisi na kanisa kwa ujumla kwa lengo la kuendeleza utumishi wa Kristo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news