NEMC YATAJA MKOA WA PWANI KUWA NA MAENEO YENYE SIFA YA KUINGIA KATIKA MTANDAO WA HIFADHI HAI DUNIANI

NA ROTARY HAULE

BARAZA la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC) kupitia kamati yake ya Kitaifa ya Binadamu na Hifadhi Hai imependekeza eneo la Rufiji,Mafia,Kibiti na Kilwa kuingia kwenye Mtandao wa Dunia wa Binadamu na Uhifadhi Hai.
Meneja wa Tafiti za Mazingira kutoka NEMC na Mratibu wa Hifadhi Hai Nchini, Rose Mtui ametoa taarifa hiyo wakati akiwasilisha mada juu ya Hifadhi Hai pendekezwa katika kikao cha kamati ya ushauri cha Mkoa wa Pwani kilichofanyika Mjini Kibaha.

Mtui amesema kuwa, Mkoa wa Pwani na Lindi ina maeneo yenye sifa ya kipekee ambayo ni fursa kubwa kiuchumi na kwa maendeleo ya jamii ndio maana kamati ya Kitaifa imependekeza maeneo hayo ili yaweze kutangazwa zaidi duniani.

Amesema, Hifadhi Hai pendekezwa ina faida za Kiikolojia ,Kiuchumi na Kijamii katika maeneo ya msitu wa Mikoko Wilaya ya Kibiti, Kilwa na Mafia,misitu ya Mwambao wa Pwani ya Mchungu,Kikale,Mto Mohoro,Mohoro ,Tambaru,Kitope na Mlola.

Amesema, faida nyingine inatokana na Hifadhi Tengefu ya Bahari,Magofu ya Kilwa (Kilwa Ruins), maeneo ya usimamizi shirikishi jamii ya wavuvi na maeneo ya ardhi oevu ya Rufiji,Mafia na Kilwa.

Aidha, amesema kuwa kupatikana kwa Hifadhi Hai hizo ambazo zitajulikana kwa jina la RUMAKI kutasaidia Kanda ya Mashariki kuwa na Hifadhi Hai kwakuwa mpaka sasa Kanda hiyo haina Hifadhi kama Kanda nyingine.

Mtui ameongeza kuwa, kwa sasa Tanzania kuna Hifadhi Hai tano ikiwemo Hifadhi ya Ziwa Manyara iliyoanzishwa mwaka 1981, Serengeti -Ngorongoro (1981),Usambara Mashariki (2000),Ghuba ya Jozani Chwaka -JCB (2016) iliyopo Zanzibar na Gombe -Masito- Ugalla (GMU) ya mwaka 2018.

"Kamati ya Kitaifa imependekeza maeneo ya Rufiji,Mafia,Kibiti,na Kilwa kuingia kwenye mtandao wa dunia wa Hifadhi Hai na hii itapelekea Tanzania kuwa na ongezeko la Hifadhi Hai kwa upande wa Kanda ya Mashariki na hata kusini,"amesema Mtui.

Amesema kuwa,uteuzi wa Hifadhi Hai hufanywa na Nchi husika lakini hupitishwa na UNESCO kwa vigezo maalum na usimamiwa na Nchini husika ambapo takwimu zinaonyesha kuwa duniani kuna Hifadhi Hai 727 katika Nchi 131 huku Tanzania zikiwa tano.

Mtui amesema kuwa,  kinachotakiwa ni kuendelea kutoa elimu kwa ngazi zote za viongozi kuanzia Kijiji,Kata,Wilaya na Mkoa pamoja na kuwashirikisha wananchi kutambua umuhimu wa kuanzisha Hifadhi Hai katika maeneo hayo.

Hata hivyo, amewaomba viongozi na watendaji waliopo katika ngazi zote kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha programu hiyo inafanikiwa kwa faida ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesifu hatua iliyofanywa na NEMC kupitia Kamati ya Kitaifa ya Binadamu na Hifadhi Hai kwa kutaka kuutangaza Mkoa wa Pwani.

Kunenge amesema kuwa, wilaya zake kuingia katika mtandao wa kidunia ni hatua kubwa ambayo itafungua fursa ya kiuchumi kwa wananchi wake na hata katika kuongeza ajira kwa vijana.

Amesema,ili jambo hilo liende sawa ni vizuri wananchi wakashirikishwa kwa kupewa elimu na ikiwezekana wataalamu watumike zaidi kutoa ushauri na mawazo yao ili kuepuka migogoro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news