Njia za kuiponya jamii na Taifa dhidi ya dawa za kulevya zatajwa

NA GODFREY NNKO

WARAIBU mbalimbali wa dawa za kulevya katika Jiji la Dar es Salaam, Tanga na Mkoa wa Morogoro wamesema kuwa,njia moja wapo za kudhibiti utumiaji wa dawa za kulevya na biashara yake ni pamoja na wazazi au walezi kufuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wao ikiwemo kuwasogeza karibu na nyumba za ibada.
Mmoja wa waraibu wa dawa za kulevya, Hussein Abdallah akitoa ushuhuda wake katika nyumba ya upataji nafuu ya Free At Last iliyopo Kihonda mkoani Morogoro.

Rai hiyo wameitoa kwa nyakati tofauti katika mahojiano na DIRAMAKINI BLOG baada ya kutaka kufahamu sababu iliyowasukuma kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya.TULETEENI TAARIFA>>>

Miongoni mwa waraibu hao aliyejitambulisha kwa jina la Aisha Said (27) mkazi wa Kata ya Mtoni iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam amesema kuwa, moja wapo ya sababu iliyochangia yeye kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya ilichochewa na mmoja wa wapenzi wake ambaye alikuwa anafika katika baa ambayo alikuwa akifanya kazi wilayani humo.

"Nilikuwa na malengo yangu mazuri kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi, Mwenyenzi Mungu alikuwa ananipatia riziki ambayo iliniwezesha kupanga chumba changu na kununua vifaa vya ndani,yule mpenzi wangu alikuwa anapenda sana kuja pale kazini, tuliweza kudumu katika mahusiano kwa kipindi cha miaka miwili, ilipofika mwaka 2017. Alikuja ofisini kwangu akaniambia 'baby wangu' sifurahishwi na kazi hii unayofanya, mimi ninaweza kukupatia kazi nzuri ambayo ina fedha nzuri, nami sikuwa na namna nilikubaliana naye, hivyo nililazimika kuacha kazi.

"Baada ya kuacha kazi,nilimfuata kwake, alikuwa amepanga chumba kimoja tu pale Zakhiem Mbagala, nilimwambia anipatie kazi ile ili niweze kufanya kwa ajili ya kupata fedha za matumizi yangu, kutumia wazazi na kulipia kodi...aliniambia, usiwe na hofu. Alinishika mkono majira ya jioni akaniambia twende nikakuonyeshe utakapofanyia kazi, tulifika Buguruni Madenge ambapo aliniingiza katika kachumba, nikamuuliza...hapa ndipo kazini, alijibu, wewe twende ndani, tulipofika huko ndani nilishangazwa na shughuli nilizokutana nazo, watu wanatoka na kuingia, tuliingia sehemu tukakuta wanapangiana hizi sigara ni za fulani na hizi ni za fulani...

"Mimi nilikaa kimya, nikisubiria nikaonyeshwe eneo la kazi. Baada ya muda, kijana mmoja alikuja akachukua sigara, huku kabla ya kuivuta akawa ameiinyoosha katika kibao chenye unga, aliivuta...mbele yetu,baada ya muda nilijihisi kichwa kinauma. Nilimuomba anirudishe nyumbani, kesho yake mchana, kichwa kilianza kunigonga sana, nikalazimika kumfauta nikamuomba anirudishe kule kwa jana, natamani nikavute ile sigara...tulipofika, nilivuta sigara ile na nilihisi kuchanganyikiwa sana,baadaye niliendelea kutamani kuivuta ile sigara ya pale pale. Nikawa siwezi kulala bila kuivuta.

"Kila nilipokuwa ninamuuliza kuhusiana na kazi alinipiga chenga na akakata mawasiliano na mimi. Wakati wangu ulikuwa mgumu sana, nilitamani kuvuta ile sigara kila wakati, nililazimika kutembea kutoka Mtongani hadi Buguruni, nilinunua na kuvuta,nililazimika kutafuta fedha kwa kila namna ili niweze kwenda kununua, nilipoona sina namna nilianza kuuza jiko langu la mchina, ndoo za maji na lile godoro langu ili niweze kununua ile sigara, mwishowe niliishiwa kabisa, mambo yakawa magumu, nilipoona sina msaada nikaamua kushirikiana na marafiki zangu kuanzia Mtoni Mtongani hadi Msikitini (Mbagala). Tunakaba, chochote kinachopatikana tunagawana, tunauza, tunaenda kupata sigara.

"Yule mwanaume sitamani kumuona tena, ndiye aliyenifanya niwe hivi,maisha yangu yamevurugika, mipango yangu imeharibika. Kila kitu kipo ovyo kwangu,"anasema Aisha Said katika mahojiano na DIRAMAKINI BLOG ambapo anaongeza kuwa, anahisi yule mwanaume alikuwa na dhamira mbaya katika maisha yake, kwani baada ya kumtumia kimwili aliachana naye tangu mwaka huo hadi leo.

TANGA

Kwa upande wake Juma mkazi wa Korogwe Mjini jijini Tanga anasema, alijikuta amejiingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya baada ya marafiki zake ambao walikuwa wanajumuika nao katika michezo ya jogging na mpira wa miguu kumuhamasisha kutumia bangi ili aweze kuwa na kasi kubwa katika michezo.

"Waliniambia nikitaka kuwa shujaa katika michezo, nivute pafu moja ya bangi, siku ya kwanza na siku ya pili niliwakatalia, lakini kila tulipokuwa tunaenda mazoezini, walikuwa wanafanya hivyo, wakawa wananiambia kuwa mimi ni mjinga, sijitambui, mwanaume muoga hawezi kuwa shujaa, maneneo yao yaliniumiza, niakaona nijaribu kuvuta, baada ya kuvuta siku ya kwanza, nilijikuta nimejiingiza katika utumiaji wa madawa (dawa za) ya kulevya, sikuwa shujaa, nilianza kudhoofika na nikatamani zaidi na zaidi kuvuta. Ninajuta kujiingiza katika utumiaji huu ambao umenisababishia kujiingiza katika matukio mabaya na wakati mwingine ninajikuta mikononi mwa polisi mara kwa mara,"anasema.

Juma anawataka wazazi kuhakikisha kuwa, wanafuatilia mienendo ya watoto wao na pale wanapobaini kuwa, wanajenga ukaribu na makundi ambayo wanaona wazi yanaweza kuharibu hatima zao au kuwaingiza katika vishawishi hatari wasione aibu kuwatenganisha.

"Watumie sana nyumba za ibada katika kuwaleta watoto wao kiroho na kiimani, utumiaji wa madawa (dawa za) ya kulevya ni mateso makubwa sana katika maisha,"anasema.

MOROGORO

Kwa upande wao, waraibu wanaopata matibabu katika nyumba ya upataji nafuu ya Free at Last iliyopo Kihonda mkoani Morogoro wamesema, chanzo kikubwa ambacho kinawafanya waraibu wa dawa za kulevya kujikuta wanaendelea kutumia dawa hizo pasipokupata msaada ni kutokana na jamii na marafiki waliowazunguka.

Hussein Abdallah amesema, alijikuta akiingia kwenye utumiaji wa dawa za kulevya kutokana na changamoto za maisha zilizompelekea kupata marafiki ambao walimshawishi na kuingia kwenye janga hilo.

"Kipindi ambacho nilikumbwa na matatizo mara baada ya kuondokewa na wazazi wangu ndipo nikajikuta nashawishika kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya,"amesema

Aidha, amesema uwepo wa Sober House umekuwa msaada mkubwa kwa waraibu wa dawa za kulevya, kwani imesaidia kupungua kwa waraibu nchini kwa maana wengi wao wamekuwa wakijiunga na sehemu ya utoaji huduma na kuweza kupona kabisa.

"Siku za mwanzo baada ya kufika hapa nilikuwa napatwa maumivu makali sana kwa sababu ya arosto, lakini wenzangu walinipa moyo na kunipa matumaini ya kuwa nitakaa vizuri,na baada ya siku kadhaa kweli mwili ukaanza kuzoea kwa maana mwanzo nilivyokuwa nyumbani sikuweza kukaa hata siku moja sijatumia dawa,"amesema.
Naye Abel Leonard ambaye anaendelea na uangalizi kutoka mkoani Mbeya anasema kuwa, hawafurahi kuwa katika hali hiyo, kwani hata yeye alijikuta ameangukia katika janga hilo baada ya kupoteza wazazi wote na kukosa marafiki wema wa kumuongoza.

Amesema, anajutia kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, kwani yamemvurugia mfumo wa maisha yake na anaamini akipona ataenda kuwa balozi mwema huko mtaani, kwa kuwa matumizi ya dawa hizo hayana faida badala yake amepoteza muda na kila kitu.

Ameyasema hayo wakati wa ziara ya waandishi wa habari wanaoendelea na kikao kazi cha siku tatu kuanzia Novemba 10 hadi 12, 2021 cha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) mjini Morogoro.

Ziara hiyo ya Novemba 11, 2021 ilikuwa sehemu ya mafunzo ambapo msimamizi wa nyumba ya Free At Last, Michael Cassian amesema, jamii ikifanikiwa kuushinda unyanyasaji na unyanyapaa kwa waathirika wa dawa za kulevya huo utakuwa ni uponyaji tosha kwao.

Pia amesema, ukosefu wa elimu sahihi kwa jamii kuhusu watu waliothiriwa na dawa za kulevya umesababisha kukithiri kwa matukio ya udhalilishaji kwa waathiriwa hao ikiwemo kuigizwa na kuitwa majina yasiyofaa kama vile mateja na mengine mengi jambo ambalo halipaswi kuungwa mkono.

"Huko mitaani jamii inatuita majina ya kila aina na wengine hata wanatuigiza jambo ambalo siyo sahihi kwani linazidi kutukandamiza sisi waathiriwa,mimi nadhani hii inatokana na jamii kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu tatizo la uraibu wa dawa za kulevya,"amesema.

WANANCHI WANASEMAJE?

Kwa nyakati wananchi waliozungumza na DIRAMAKINI BLOG jijini Dar es Salaam ilipotaka kufahamu ni sababu gani inayochochea vijana kujiingiza katika utumiaji na uuzaji wa dawa za kulevya na nini kifanyike wamesema kuwa, jambo muhimu ni vijana kujitambua.

"Suala la msingi, vijana wanapaswa kujitambua na kujithamini. Ukishindwa kujitambua utajikuta unapelekeshwa na upepo, ninafikiri hii ni moja wapo ya sababu kubwa inayochangia kuongezeka kwa watu wanaotumia dawa za kulevya.

"Jambo la msingi vijana wafanye kazi kwa bidii, waache tabia za kukaa vijiweni bila kujishughulisha, kwani kukaa ovyo ovyo ni kichocheo moja wapo cha kujiingiza katika utumijia wa dawa za kulevya na hata biashara hiyo ambayo haina nyuma wala mbele. Pia niiombe Serikali iendelee kutoa elimu kwa spidi sana kuhusu madhara yatokanayo na utumiaji wa dawa za kulevya kuanzia vijijini hadi mijini,"anafafanua Pascal Damas mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam.

Said Juma Said mkazi wa Ilala anasema, dawa za kulevya ni janga hatari katika jamii na Taifa, hivyo ili kuwanasua vijana katika dimbwi hilo ni vema Serikali ikaratibu mpango maalumu utakaosimamiwa na watu sahihi ambao utawezesha vijana kujihusisha katika biashara ndogondogo katika maeneo yanayowazunguma na elimu iendelee kutolewa kila siku.TIBA KWA WAATHIRIKA>>>

WATUMISHI WA MUNGU

Watumishi wa Mungu akiwemo Rais wa New Covenant Unity International (NCUI) ambaye pia ni Kiongozi wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Dkt.Joshua Aram Mwantyala amesema kuwa,si jukumu la Serikali pekee au wazazi kuwanasua vijana katika utumiaji au biashara za dawa za kulevya nchini.

Dkt.Joshua anasema kuwa, ushirikiano baina ya Serikali,wazazi na watumishi wa Mungu ni njia moja nyepesi na ya haraka inayowezesha kuwanasua vijana katika utumiaji wa dawa za kulevya hususani katika Dunia hii ya utandawazi.

Anasema, katika Dunia hii ya utandawazi ambayo mambo mengi yanafanyika katika kiwango cha kimataifa, na kukihamisha nje ya mipaka na kukifanya kuwa cha wazi na kikafanywa na watu wa aina yote duniani, mapokeo yake yameendelea kuwa na athari chanya na hasi.

Nabii Dkt.Joshua anasema, athari hasi ni pamoja na mapokeo ya vijana kuutumia utandawazi huo ambao mataifa yanafanya mambo yake hadharani katika nyanja mbalimbali kama vile biashara, uchumi au siasa uliowezeshwa na maendeleo ya teknolojia ya habari yanayofanya mataifa kuwasiliana kiurahisi, kutenda mambo ambayo yana madhara makubwa ikiwemo utumiaji wa dawa za kulevya.

"Utandawazi huu pia umelenga katika kumiliki fikra au tamaduni zilizo dhaifu kama hizi za watu kuiga tabia za utumiaji wa dawa za kulevya, hivyo ili tuweze kuushinda utandawazi ni pamoja na sisi watumishi wa Mungu kusimamia imara katika kuwaunganisha vijana na Watanzania kwa kuwahubiri neno sahihi la Mungu na kuwaonyesha njia bora za kufanikiwa wakiwa ndani ya Mungu kuliko kutegemea mambo ya Dunia.

"Tunapaswa kuwajenga imara vijana ili wasijiingize katika mienendo mibaya kwa sababu ndio wana nguvu ya kupigana vita vya kimwili na kiroho. Ukisoma 1Yohana 2:14 inasema "Nimewaandikia vijana kwa sababu mna nguvu na neno la Mungu linakaa ndani yenu nanyi mmemshinda yule mwovu, msiipende dunia wala mambo yaliyomo katika dunia, kwa sababu ukiipenda dunia kumpenda baba hakumo ndani yako,"anafafanua Dkt.Joshua.

NGUVU ZA KIROHO

Nabii Dkt.Joshua anasema, nguvu za kiroho zinaweza kubadilisha fikra zilizoathiriwa na mambo magumu kama ilivyoelezwa kitabu cha Waefeso 6:10-18, kwa sababu ukweli ndio utamweka kijana kuwa huru na kuwa na uamuzi juu ya mustakabali wa maisha yake.

"Hivyo kijana akijua faida ataweza kukimbizana nazo ili apate kufaidika nazo na akijua hasara zake pia atajiepusha na kubaki katika hali nzuri aliyoumbwa nayo. Hivyo ili kuwanasua vijana katika haya matumizi ya dawa za kulevya, sisi watumishi wa Mungu,wazazi, walimu,vyombo vya habari, jamii na Serikali tunapaswa kuwa muongozo sahihi na kioo kitakachowanasua vijana katika hizi changamoto.

"Wengi wa vijana ambao wametumbukia katika utumiaji wa dawa za kulevya ukiwachunguza vizuri utagundua kuwa wamekosa malezi bora, upendo, wazazi hawajali, jamii haijali shida zao, walimu wanawabagua, vyombo vya habari vinawabeza au vinapitisha maudhui ya kuwachochea kujiingiza huko. Sisi tusimame imara kwa kwa sababu upendo wa Mungu unatosha.

"Ndiyo maana unaweza kuona tofauti kubwa kati ya kijana anayejiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya au maovu na upande mwingine kijana anayechagua kujiheshimu na kusimama imara bila kutikiswa na mambo mabaya huwa anapata mafanikio makubwa mno,"anasema Nabii Dkt.Joshua.

Pia Nabii Dkt. Joshua anasema kuwa, ukisoma katika kitabu cha Mathayo 11:28-30, utaona nguvu iliyopo katika kumtegea Mungu.

“Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu; jifunzeni kutoka kwangu; kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. Kwa maana nira yangu ni rahisi, na mzigo wangu ni mwepesi.”

Nabii Dkt. Joshua anahoji kuwa, je? Kijana, utandawazi umekulemea? Umekuwa mzigo kwako? Umekuachia majeraha? Umekuachia mazoea mabaya? Umeona umenyimwa haki au umeonewa? Shaka ondoa na usijiingize katika utumiaji wa dawa za kulevya kutafuta faraja, faraja pekee inapatikana kwa Mungu, njooni kwake ili mnusurike na mambo mabaya ya kidunia.

DOTTO MNYADI

Wakati huo huo, imeelezwa kuwa, tabia ya kutozungumza unapokuwa na tatizo ni miongoni mwa sababu inayotajwa kuwachochea vijana wengi kutumbukia kwenye matumizi ya dawa za kulevya.
Dotto ameyasema hayo wakati akitoa mada kwenye mafunzo maalumu kwa wanahahabari kuhusu dawa za kulevya yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) yaliyofanyika kwa siku tatu mkoani Morogoro.

Mkufunzi mwandamizi wa maudhui ya kidigitali, Dotto Mnyadi amesema kuwa, familia nyingi zimekuwa na tabia ya kutozungumza mara kwa mara na kuwaacha vijana hususani waliokuwa kwenye rika balehe kujisimamia bila miongozo ya karibu na upendo wa familia.

"Kuna tabia zisizofaa ambazo zinapaswa kubadilishwa,utakuta kwenye familia hawana muda hata wa kujua matatizo anayopitia mtu,hawaongei nini, na utakuta mtu anapitia kipindi kigumu, lakini anajikaza, anasema huo ndio umwamba mwisho wa siku anapotea,"amesema.

USHAURI KWA SERIKALI

Wakati huo huo, Serikali imeshauriwa kuja na mpango mkakati wa kuliweka suala la dawa za kulevya kwenye mitaala ya elimu kuanzia ngazi ya msingi kutokana na stadi zilizofanyika kubaini kuwa kuna tatizo kubwa kwenye shule za msingi.

Ni kwa kuwa watoto wanaanza kutumia dawa hizo mpaka wanapofikia sekondari au vyuo wanakuwa tayari wameshakuwa waathirika wakubwa wa tatizo hilo.

Ushauri huo umetolewa na Irene Kaoneka ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya CASA FAMILIA ROSSETA inayojihusisha na kulea watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi pamoja na kusaidia watu wenye mahitaji maalumu.

Amesema, hivi karibuni wameweza kufanikisha kampeni ya kupambana na dawa za kulevya kwa kushirikisha midahalo mbalimbali kwenye shule zaidi ya 38 jijini Tanga ikiwemo shule ya Sekondari Galanosi.

Mkurugenzi Irene amesema, ipo haja ya serikali kuja na mpango huo ili kunusuru vizazi vijavyo na kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya kwani watajapokutana na somo hilo kuanzia ngazi ya shule ya msingi itasaidia wao kujitambua na kujua madhara yake kwa haraka.

Amesema, vijana wengi walio kwenye uraibu wa matumizi ya dawa za kulevya walianzia wakiwa kwenye elimu ya msingi, hivyo ni vyema Serikali ikawliweka suala hilo kwenye mitaala ya kielimu, lengo likiwa ni kuwafundisha elimu ya kujitambua mapema.

Pia Mkurugenzi huyo ametoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kuwanyanyapaa watumiaji wa dawa za kulevya na badala yake amewataka wawasaidie kuwapeleka katika vituo vitakavyowasaidia kupata utabibu.

Naye daktari aliyebobea katika masuala ya afya ya akili kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tanga-Bombo, Dkt. Wallace Karata amesema kuwa, katika kampeni wanazofanya wamelenga shule za sekondari kwa kuwa ndio wanafunzi wanaoweza kujipambanua ili kuwalinda watoto wa shule za msingi.

"Tumelenga zaidi shule hasa ngazi ya sekondari kwa kuwa hawa ndio wanaonekana kuwa kwenye hatari zaidi kuliko makundi mengi na tunazunguka kuwapatia elimu hii, hivyo niwaombe vijana waachane na tabia hii ya matumizi ya dawa za kulevya,"amesema Karata.

Dkt.Karata anasema kuwa, Mkoa wa Tanga ni mkoa wa pili kwa matumizi ya dawa za kulevya hivyo ipo haja ya kuendelea na mapambano dhidi ya dawa hizo wakiamini elimu na midahalo ambayo wamekuwa wakiifanya itakuwa njia bora ya kuisadia jamii, hivyo wameomba kuungwa mkono.UVUTAJI SHISHA NI HATARI>>>

WANAFUNZI WANASEMAJE?

Kwa upande wao, wanafunzi akiwemo Iddy Jumanne na Innocent Patric, Asha Ramadhani, Rose Michael wameiomba serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kuja na mpango kabambe wa kufikisha elimu kuanzia ngazi za chini kuhusu athari, namna ya kuwatambua watumiaji wa dawa za kulevya na jinsi ya kufikisha taarifa kwa mamlaka pindi wanapobaini watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Rose Michael ambaye ni miongoni mwa wanafunzi hao kutoka jijini Tanga ameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, hatua hiyo itasaidia kuwafichua kwa haraka wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya.

"Kama vile Jeshi la Polisi linaendesha dawati la jinsia na watoto, vivyo hivyo mamlaka inayohusika na kupambana na dawa za kulevya (Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya-DCEA) ije na dawati la siri au kuanzisha namba maalumu ya simu kwa ajili ya kuwasilisha taarifa zinazohusiana na wafanyabiashara, watumiaji na maeneo wanakofanyia biashara hizo ili waweze kuziokoa familia zetu katika maangamizo haya,"amesema Rose Michael katika mahojiano na DIRAMAKINI BLOG.

WALIMU WANASEMAJE?

Kwa yakati tofauti walimu kutoka shule za msingi na sekondari jijini Tanga na Dar es Salaam wameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa,licha ya nafasi yao ya malezi ambayo wanayatoa kwa watoto wao wawapo shuleni, ushirikiano kati yao na walezi au wazazi wa watoto hao ni muhimu sana katika kufuatilia mienendo ya watoto wao.

Justine Mwita ambaye anasema ni miongoni mwa walimu wa shule ya msingi katika Jiji la Ilala, Dar es Salaam anasema kuwa,ukaribu na malezi bora ni tiba tosha kwa watoto, hivyo ni jukumu pia la wazazi kuongeza ukaribu katika kufuatilia mienendo ya watoto wao wawapo nyumbani, wanapoenda shule, wanapocheza ili kuweza kufahamu changamoto zinazowakabili.

"Wakati mwingine wazazi wamekuwa ni sehemu ya changamoto kubwa ambayo imesababisha maumivu na mienendo mibaya kwa watoto wao, badala ya kufuatilia mienendo ya watoto wao hususani aina ya marafiki wanaocheza nao au wanaoambatana nao nyumbani,wamekuwa wapo 'busy' sana katika mambo yao ya nyumbani, mwisho wa siku unakuta marafiki wabaya wamebadili fikra za mtoto na kumuingiza aina ya tabia za ovyo ovyo, hadi kupelekea kujiingiza katika matendo mabaya kama matumizi ya dawa za kulevya,"anasema Mwalimu Mwita.

Mawazo ya mwalimu huyo yanaenda sambamba na ya mwalimu Leonard Ojoi wa Shule ya Galanosi Sekondari ambaye anasisitiza kuwa, njia moja wapo ya kukata mnyororo wa watoto kujiingiza katika mienendo mibaya kama matumizi ya dawa za kulevya mi pamoja na wazazi kushirikiana bega kwa bega na walimu kufuatilia mienendo ya watoto wao wawapo nyumbani na shuleni.

Anasema kuwa, mara nyingi watu wenye nia ovu kama vile watumiaji au wauzaji wa dawa za kulevya huwa wanajenga mazingira makubwa kwa watoto wadogo ili iwe rahisi kufanikisha mipango yao ya biashara na utumiaji wa dawa hizo haramu.

JUHUDI

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ipo katika mpango wa kutengeneza miundombinu rafiki yya ajira kwa waraibu ambao wanatoka katika matibabu ili wasiweze kupata ushawishi wa kurudia matumizi yya dawa za kulevya.
Kamishina wa Tiba na Kinga wa DCEA, Dkt.Peter Mfisi amesema, kumekuwa na baadhi ya waraibu wamekuwa wakirudia kutumia dawa za kulevya kutokana na mazingira ambayo wanakutana nayo pindi wanapotoka kupata matibabu.

Amesema, watakaa na wizara kuona ni namna gani wanaweza kutatua changamoto wanayokutana nayo waraibu ambao wameshapata matibabu hasa kuona nini wafanye ili wakishatoka katika matibabu iwe rahisi kupata ajira ambayo iatweza kumsaidia kujikimu kimaisha na kuondokana na kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya.

Pia ameitaka jamii kutowanyanyapaa hususani wanawake, kwani utafiti umeonesha kuwa kati ya wanawake 100 wanaotumia dawa za kulenya nchini 61 kati yao wameambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU) kutokana na kuchangia sindano za kujidunga.

Dkt.Mfisi anasema, utafiti huo ulifanyika mwaka 2014 ambapo mpaka sasa bado haujafanyika utafiti mwingine ili kujua ukubwa wa tatizo.

Amesema kuwa, kutokana na tatizo hilo,DCEA imejipanga kuanzisha kliniki maalumu za waraibu wa dawa za kulevya zitakazowasaidia waraibu wanawake kupata matibabu kwa wakati na kliniki hiyo itawaondolea tatizo la kuwa na hofu ya kunyanyapaliwa.

Kamishina huyo amesema kuwa, lengo kuu la kikao kazi hicho ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari za Kidigitali kuihabarisha jamii ya Kitanzania hususani waathirika wa dawa za kulevya pamoja na VVU ili kuchukua hatua stahiki za kimatibabu.

“Lengo kuu la kikao kazi hiki ni kutaka kuifikia jamii kupitia ninyi wanahabari ili kuihabarisha jamii ifahamu juhudi za mamlaka katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya na nini wanapaswa kufanya hasa wanapoona kuna waathirika miongoni mwao. Pia kusaidia kutafuta mbinu za kuwashawishi wanawake wafike kwenye maeneo ya tiba na kujiunga na vituo vya matibabu, maana tunajua wapo na wameathirika na dawa za kulevya, lakini kwa sababu ya unyanyapa wanaogopa kujitokeza katika vituo,"amesema Dkt.Mfisi.

Wakati huo huo,Dkt.Mfisi amesema, kwa sasa idadi ya wanawake wanaotumia dawa za kulevya wanaokwenda katika vituo vya matibabu ni wachache.

"Kwa mfano ukiangalia katika Sober House (nyumba za upataji nafuu) unakuta kiwango cha wanawake wanaojitokeza kupata matibabu ni kidogo sana na hata ukichukua ile jumla ya matibabu wanawake bado wako chini ya asilimia tano. Katika kliniki nyingine unakuta wako asilimia tatu au asilimia nne kwa uwakilishi wa wanawake ni mdogo.

"Pia hawaendi kwenye vituo vya matibabu, kwa hiyo mamlaka tuna kila sababu ya kuweka vituo maalumu ili kuwafanya wanawake nao wajitokeze katika matibabu kwa wale ambao wamekuwa na uraibu wa dawa za kulevya, sehemu ya vivutio hivyo labda kutafuta kliniki itakayokuwa na mahitaji maalum ya wanawake ili wajitokeze kwa wingi.

Kamishina huyo amesema kuwa, kliniki hizo zitakuwa na uwezo wa kuwahudumia watoto wadogo waliozaliwa na uraibu na ambao kwa kiasi kikubwa huwa wanazaliwa wakiwa na tatizo la arosto kutokana na matumizi ya dawa za kulevya kwa mama mjamzito.

"Watoto wengi wanaozaliwa na akinamama wanaotumia dawa za kulevya wanakuwa na arosto, kliniki hizo zitakuwa na uwezo wa kuwasaidia watoto wote waliozaliwa na tatizo hilo.Pia kliniki hizo zinaweza kuwa na meneo ya kucheza watoto, kama mama amekuja na mtoto basi anampeleka kucheza au kunakuwa na elimu ya mama na mtoto, inakuwa zaidi ya ile kliniki ambayo mama anakwenda na kuondoka , ukiacha kutibu hiyo arosto ambayo mtoto anakuwa nayo, lakini kunakuwa na vitu vingine,"amesema.

Dkt.Mfisi amesema, pia kuna baadhi ya wanawake wanashindwa kwenda kupata matibabu kwa sababu ya muda, kwani mara nyingi matibabu yanaanza saa kumi na mbili asubuhi hadi saa tano asubuhi.

"Kutokana na changamoto hiyo, tunadhani ni vema wakaangalia na muda mwingine ili wawepo wanaokwenda asubuhi na wanaokwenda jioni kulingana na ratiba zao ili waweze kupata matibabu,"amesema.

MRAIBU ANAPELEKWA JELA?

Kamishna wa Tiba na Kinga wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya,Dkt.Peter Mfisi amesema, sheria inatambua kuwa uraibu ni ugonjwa, hivyo hukumu pekee ni kumpeleka mraibu hospitali na siyo jela kama jamii inavyofikiria.

Dkt.Mfisi anasema kuwa,Jeshi la Polisi limekuwa likitumia weledi mkubwa wanapowakamata waraibu wa dawa za kulevya ambapo hushirikiana na familia zao kuwasainisha matibabu ya lazima ya kuondokana na uraibu kwa muda wa miezi sita.

"Jambo la kushangaza,wengi wao wamekuwa hawafuati adhabu hiyo na kurudi kwenye matumizi ya dawa hizo haramu,"amesema.

Dkt.Mfisi anasema kuwa, adhabu hiyo ni kwa wale waraibu wanaokamatwa na makosa ya kukutwa wakitumia dawa hizo na siyo wale wanaokamatwa wakifanya uhalifu mwingine baada ya kutumia dawa za kulevya.

"Kwa hao wengine wanaokamatwa kwa tuhuma za wizi au kumdhuru mtu,sheria huchukua mkondo wake kama kawaida ila nafikiri wakati mwingine polisi hutumia busara na kulazimika kuwaachia kutokana na hali zao kiafya kushindwa kuhimili kukaa mahabusu kwa muda mrefu hususani wanapopatwa na arosto,"ameongeza

DCEA

Wakati huo huo Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema kuwa, kila Mtanzania ana wajibu wa kutoa taarifa yoyote inayohusiana na uhalifu wa dawa za kulevya hapa nchini.

"Mamlaka tunafanya kazi kutokana na jamii. Kwa niaba ya Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Gerald Kusaya niwahakikishie kuwa, mtu au watu ambao wataleta taarifa zao katika mamlaka zinazohusiana na uhalifu wa dawa za kulevya, tutazipokea kwa uaminifu wa hali ya juu na tutamtunzia siri, hivyo msiwe na hofu yoyote kama mna taarifa.

"Nirejee wito huu kwamba, endeleeni kutuma au kuleta moja kwa moja taarifa zinazohusiana na uhalifu wa dawa za kulevya, zitapokelewa kwa usiri mkubwa na kufanyiwa kazi;

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka DCEA, Florence Khambi aliyasema hayo katika kikao kazi na waandishi wa habari kilichoandaliwa na mamlaka hiyo mkoani Morogoro kwa siku tatu wakati akielezea kuhusiana na mamlaka hiyo katika siku ya kwanza.

Mkuu huyo amebainisha kuwa, dawa za kulevya ambazo ni tatizo kubwa hapa nchini ni pamoja na bangi na mirungi.

Kwa sheria ya Tanzania, mtu ukifanya kilimo cha dawa za kulevya mfano ukilima bangi na mirungi (dawa za mashambani) au ukikutwa na mbegu zake, ukikutwa na hatia adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 30 na kosa hili halina dhamana.

Hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya namba 5 ya mwaka 2015 ambayo ilianza kutumika kuanzia Mwezi Septemba 2015 na kurejewa mwaka 2019.

Wakati huo huo, Khambi amesema kuwa, dira yao kama mamlaka ni kujenga jamii ya Tanzania isiyotumia dawa za kulevya au kushiriki katika biashara ya dawa hizo na hivyo kuchangia lengo kuu la kuwa na maisha bora nchini kama ilivyochagizwa kwenye malengo ya maendeleo ya 2025.

"Na dhima yetu ni kujenga mfumo bora wa kudhibiti na kupambana na matumizi na biashara ya dawa za kulevya na kuendeleza ushirikiano katika hatua mbalimbali za udhibiti wa dawa za kulevya na kujenga uwezo wa taasisi na asasi zisizo za kiserikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya,"amefafanua.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka DCEA, Florence Khambi amesema, majukumu ya mamlaka ni kufafanua, kuhamasisha, kuratibu na kutekeleza hatua zote zinazoelekezwa katika udhibiti wa dawa za kulevya.

"Hivyo, katika kutekeleza majukumu hayo mamlaka inafanya kazi ya kusimamia utekelezaji wa mikataba ya Kimataifa, maazimio na makubaliano katika kudhibiti dawa za kulevya, kuandaa na kutekeleza mpango wa Taifa wa kudhibiti dawa za kulevya,"amesema.

Khambi amesema kazi nyingine ni kutengeneza miongozo inayoelezea tatizo la dawa za kulevya na madhara yake katika jamii.

"Pia kuboresha na kurekebisha sheria na kanuni za udhibiti wa dawa za kulevya,kuhamasisha udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya ikiwemo kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya, kusambaza taarifa kwa umma na juhudi nyingine za udhibiti.

Na kazi nyingine ni kuchukua hatua stahiki za kupambana na biashara ya dawa za kulevya zikiwemo kukamata, kupekua na uchunguzi wa masuala yanayohusiana na dawa za kulevya.

"Pia kuzuia, kupeleleza na kuchunguza uchepushaji wa dawa za tiba zenye madhara ya kulevya pamoja na kemikali zilizosajiliwa kutoka kwenye vyanzo halali wakati huo huo kuhakikisha dawa hizo zinapatikana kwa matumizi ya tiba, biashara na mahitaji ya kisayansi na kuanzisha mfumo thabiti wa ukusanyaji taarifa na uchambuzi katika ngazi ya taifa kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya,"amesema.Khambi ameendelea kufafanua kuwa, kazi nyingine ya DCEA ni kuhamasisha, kuratibu na kuhakikisha jitihada za ushirikiano wa kimataifa katika kudhibiti wa dawa za kulevya zinaimarishwa na kufanya, kuwezesha na kuratibu tafiti zinazohusiana na dawa za kulevya.

"Mamlaka pia inajishughulisha na kazi ya kuratibu na kuwezesha wadau wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya, kuelimisha na kuhamasisha jamii kushiriki katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

"Kutoa mafunzo kwa watendaji wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya, fedha haramu na kemikali bashirifu na kufanya uchunguzi wa sayansi jinai,"amefafanua Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka DCEA, Florence Khambi wakati akielezea kuhusiana na DCEA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Aisee hili ni bonge la makala. Hongereni sana kwa andiko nzuri ingawa ni refu sana

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news