Njooni muwekeze hapa Mbeya, fursa zipo nyingi-DC Chuachua

NA DOREEN ALOYCE

KATIKA kuendeleza jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza utalii na uwekezaji hapa nchini, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Daktari Rashidi Chuachua amesema ni fursa kwa wawekezaji kwenda kuwekeza ndani ya Jiji hilo na mkoa kutokana na kuwepo kwa fursa nyingi za kiuchumi ikiwemo maeneo makubwa ya kilimo,ufugaji na viwanda.
Aidha, amesema Jiji la Mbeya ni miongoni mwa majiji makubwa hapa nchini ambayo hali ya hewa na mandhari ni nzuri kwa uwekezaji ambapo pia miundombinu ya barabara,maji,umeme vimeboreshwa.

Daktari Chuachua ameitoa kauli hiyo jijini Mbeya wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wanawake kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini waliofika jijini hapa kufanya ziara ya kutangaza vivutio vya utalii na uwekezaji vilivyopo jijini hapa.

Amesema kuwa, kutokana na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio na uwekezaji vilivyopo hapa nchini kama wasaidizi wake hawana budi kumuunga mkono kwani ndani ya Tanzania kuna uwekezaji mkubwa na maeneo yenye vivutio, lakini bado havijatangazwa ipasavyo.

"Niwapongeze sana waandishi wa habari wanawake kwa maamuzi yenu ya kumuunga mkono Rais wetu Samia Suluhu Hassan inaonyesha ni kiasi gani mlivyo wazalendo juu ya nchi yenu, na najua tukishikamana kwa pamoja tutapata mafanikio makubwa kwani wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi watakuja kuwekeza na kutembelea vivutio vyetu.

"Mfano hapa ndani ya Jiji la Mbeya kuna vivutio vikubwa na vidogo ambavyo wageni wakifika watafurahia sana hasa mlima Mbeya,Ziwa Ngozi, Nyumba ya Binti Matola ambayo ilitumika kumhifadhi Hayati Mwalimu Julias Nyerere alipofika kwa ajili ya harakati za kupigania uhuru,vituo vidogo walivyokuwa wakitumia wakoloni pamoja na Shule ya Sekondari Lozera ambapo kuna vivutio,"amesema Dkt.Chuachua.

Ametoa wito kwa Watanzania kuwaunga mkono waandishi wa habari wanawake ambao wameanza vizuri kuutangaza uwekezaji na utalii jambo ambalo litasaidia kuibua fursa zilizopo na itasaidia kukuza uchumi wa Nchi na mtu mmoja mmoja na kukuza ajira kwa Watanzania.

Ndele Mwasesela ambaye ni Mkurugenzi wa shule ya awali na Msingi ya Paradise Mission Ndele Mwaselela iliyopo mkoani Mbeya amesema, tayari amewekeza Sekta ya elimu jijini Mbeya ambapo wazazi wana mwitikio mkubwa kuwasomesha watoto wao na kwamba atakuwa bega kwa bega na wanahabari hao kutangaza fursa zilizopo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi jijini Mbeya wamewashukuru waandishi wa habari wanawake kwa kuja kutembelea mkoa huo na kutangaza fursa za uwekezaji na utalii ambapo walibainisha kuwa endapo koa huo utatangazwa vizuri na mazingira ya uwekezaji yakaboreshwa yatasaidia mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa inayochangia zaidi pato la Taifa.

Anna Mangia amesema, miongoni mwa fursa katika uwekezaji zilizopo ni pamoja na uchakataji wa mazao mbalimbali ikiwemo mchele,mbogamboga, matunda kama vile parachichi na ndizi mbivu.

Hivyo ameiomba serikali kuunga mkono juhudi za waandishi wa habari wanawake katika kutangaza fursa hizo kwa kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi yatakayokuwa rahisi kwa muwekezaji kufanya uwekezaji wake ikiwemo suala la vibali na kuondoa kodi ambazo ni vikwazo kwa wawekezaji.

Awali Mratibu wa kampeni ya wanahabari wanawake kutoka mikoa mbalimbali ya kutangaza utalii na uwekezaji nchini, Mary Mwakibete,amesema lengo la kuanzisha kampeni hiyo ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kutangaza utalii pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Amesema,kampeni hiyo ilianza Agosti,2021 kwa kutembelea Mkoa wa Iringa hivyo kwa Mkoa wa Mbeya ni awamu ya pili na wataendelea hivyo kwa mikoa mingine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news