NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesisitiza haja kwa Wakaguzi wa Ndani kujikita zaidi kwenye utendaji badala ya kuishia kwenye vitabu hatua ambayo itasaidia kujua jinsi ya matumizi ya fedha yanavyofanyika.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Novemba 29,2021 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani nchini Tanzania ulioongozwa na Rais ambaye pia, ni Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Bi. Zelia Njeza.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akipokea Kitabu cha Muongozo wa Kimataifa kwa Waguzi wa Ndani kutoka kwa Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIAT), Zelia Njeza baada ya mazungumzo na ujumbe wa taasisi hiyo walipofika Ikulu jijini Zanzibar pamoja na kupokea pongezi kwa uongozi wake wa mwaka mmoja. (Picha zote na Ikulu).
Katika maelezo yake, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kwamba ni vyema Wakaguzi wa Ndani kuifanyia ukaguzi miradi husika badala ya kuishia kwenye vitabu hatua ambayo ambayo itasaidia kuondosha baadhi ya changamoto zinazojitokeza hivi sasa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (katikati) alipokuwa akizungumza na Ujumbe wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIAT) unaoongozwa na Rais wa taasisi hiyo,Zelia Njeza (wa tatu kushoto) walipofika Ikulu jijini Zanzibar pamoja na kupokea pongezi kwa uongozi wake wa mwaka mmoja.
Rais wa Zanzibar ameahidi kufanya kazi na taasisi hiyo ili Zanzibar iweze kupiga hatua kwa kiasi kikubwa katika suala zima la Ukaguzi wa Ndani.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi alieleza kwamba kuwepo kwa taasisi hiyo kutasababisha na kuwasaidia Wakaguzi wa Ndani kupata mafunzo pamoja na kutambulika.
Amesema kuwa, kuwepo kwa wakaguzi wa ndani ni jambo lenye umuhimu katika taasisi za Serikali jambo ambalo limekuwa likitiliwa msisistizo kwani mara nyingi ripoti za ndani huwa haziridhishi hiyo ni kutokana na wakaguzi wa ndani kutokuwa na nguvu.
Ametoa pongezi kwa mafanikio ya jumla ya taasisi hiyo na kueleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kufanya kazi na taasisi hiyo kwa azma ya kupata mafanikio zaidi.
Pamoja na hayo, Rais Dkt.Mwinyi ametoa pongezi kwa taasisi hiyo kwa uamuzi wake wa kutoa mafunzo kwa Makatibu Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hatua ambayo itasaidia kupata uwelewa wa pamoja na kusisitiwa uwepo wa Wakaguzi wa Ndani katika mafunzo hayo.
Amesisitiza kwamba bila ya kuwepo kwa usimamizi mzuri wa Ukaguzi wa Ndani, wa fedha za UVIKO-19 zinazotarajiwa kutolewa fedha hizo zinaweza zikapotea hivyo, ni vyema watendaji hao wakapewa mafunzo ili kupata matokea mazuri ya usimamizi wa fedha hizo.
“Kila taasisi inayopokea fedha za UVIKO-19 ni vyema ikawa na ushiriki wa karibu sana na Wakaguzi wa Ndani ili kuepuka athari zinazoweza kuja kutokea hapo baadae,”amesisitiza Dkt.Mwinyi.
Sambamba na hayo, Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza juu ya suala zima la maadili katika fani ya Ukaguzi wa Ndani hasa ikifahamika kwamba kada hiyo ina umuhimu mkubwa katika utekelezaji wake sanjari na ushirikishwaji wa Taasisi hiyo na Vyuo vinavyosomesha kada hiyo.
Naye Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said alieleza umhimu wa wanachama wa taasisi hiyo kuwa na elimu zaidi ya kada hiyo sambamba na kueleza jinsi Serikali ilivyopokea mafunzo ya Ukaguzi wa Ndani yatakayotolewa na taasisi hiyo na kueleza kwamba yana umuhimu mkubwa kwa viongozi hao.
Mapema Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani nchini Tanzania, Bi.Zelia Njeza alitoa pongezi kwa Rais Dkt. Mwinyi kwa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wake akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Aidha, katika maelezo yake kiongozi huyo ambaye amefuatana na wajumbe wa taasisi hiyo kutoka Zanzibar na Tanzania Bara alieleza kwamba taasisi yao iliyoanzishwa mwaka 2006 iko kisheria na inafuata taratibu zote ziliwekwa ikiwa na lengo la kuimarisha kada ya Ukaguzi wa Ndani nchini.
Bi Zelia Njema alisisitiza kwamba iwapo nchi inataka kuimarisha suala zima la utawala bora basi ni vyema suala la ukaguzi wa ndani likapewa nafasi yake huku akieleza azma ya taasisi hiyo ya kutoa mafunzo kwa Makatibu Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya Ukaguzi wa Ndani.
Pia, aliongeza kuwa nchi inaweza kupata maendeleo makubwa ya kiuchumi iwapo Ukaguzi wa Ndani ukapewa kipaumbele na kueleza Tanzania jinsi ilivyopiga hatua kwenye suala hilo katika nchi za Afrika kwa kufanya kazi vizuri ikitanguliwa na Afrika Kusini.
Sambamba na hayo, taasisi hiyo ilieleza mafanikio iliyoyapata pamoja na changamoto zinazojitokeza huku ikieleza namna inavyochukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi.