Rais Dkt.Mwinyi atoa maelekezo kwa Chuo Kikuu Huria kuhusu mitaala

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

CHUO Kikuu Huria cha Tanzania kimetakiwa kuangalia mitaala yake jinsi itakavyosaidia kuandaa wataalamu watakaoweza kutekeleza dhamira ya kujenga uchumi mpya unaozingatia matumizi ya rasilimali za bahari au uchumi wa Buluu ambao ni ajenda maalum ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane.
Wahitimu wa Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Miradi (Master of Project Management) wakitunukiwa Shahada yao na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Pinda (hayupo pichani) wakati wa mahafali ya 40 ya chuo hicho yaliofanyika katika Uwanja wa Mao Zedung jijini Zanzibar Wilaya ya Mjini Unguja, Novemba 25,2021.(Picha zote na Ikulu).

Rai hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika Mahafali ya 40 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika katika uwanja wa Mao Ze Dong jijini Zanzibar, Novemba 25, 2021 ikiwa ni Mahafali ya kwanza kufanyika hapa Zanzibar tokea kuanzishwa kwa Chuo Kikuu hicho mnamo mwaka 1992.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akishiriki katika Maandamano ya Mahafali ya 40 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania, wakati wa hafla hayo yaliofanyika katika uwanja wa Mao Zedung jijini Zanzibar na kushoto kwa Rais ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe.Simai Mohammed Said.  

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi alikihimiza Chuo Kikuu hicho ambacho Mkuu wake ni Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Kayanza Peter Pinda, kufanya tafiti zenye lengo la kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii katika nyanja zote za maendeleo.

Amesema kuwa, kufanya tafiti ni moja ya majukumu ya msingi ya Vyuo Vikuu na matokeo ya utafiti yawafikie watu na yawe na manufaa kwao.

Akiwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Rais Dkt.Mwinyi alitoa rai kwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuangalia maeneo ya ushirikiano kati yake na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Mahafali ya 40 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania yaliofanyika katika Uwanja wa Mao Zedung jijini Zanzibar na kushoto kwa Rais ni Prof.Deus Ngaruko ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma) na Prof.Elifas Bisanda Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania.

Aliyataja maeneo ya ushirikiano katika masuala mbalimbali hasa utafiti,Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), mbinu za kisasa za ufundishaji na kutafuta fursa za ajira nje ya nchi kwa wahitimu wa shahada za lugha ya Kiswahili zinazotolewa na vyuo hivyo.

Alikitaka chuo hicho kutumia changamoto walizonazo kuwa ni fursa na wala zisiwakatishe tamaa katika kufikia Dira na Malengo ya kuanzishwa kwa chuo hicho.

Amesema kuwa, kufanyika kwa mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa mara ya kwanza hapa Zanzibar sio tu kuna umuhimu wa kihistoria kwa chuo hicho bali pia, ni hatua muhimu katika kuimarisha Muungano wa Tanzania kwa dhamira ile ile ya waasisi wa Taifa hili Hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Aliongeza kuwa hiyo ni fursa nyingine ya kuimarisha na kuendeleza umoja wa Watazania baada ya chuo hicho kuanzisha matawi yake hapa Unguja mwaka 1995 na kule Pemba mwaka 2004, na kupongeza kazi nzuri ya chuo hicho tokea kuanzishwa kwake ambapo wanafunzi wapatao 4,534 wamedahiliwa kutoka Zanzibar katika programu na ngazi mbalimbali.

Rais Dkt.Mwinyi alisema kuwa, alisema kuwa kati yao wapo waliohitimu na walisema kuwa wapo viongozi mbalimbali wa Serikali ambao ni matunda ya chuo hicho na kupongeza kazi nzuri inayofanwya na chuo hicho.
Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Pinda akimtunuku Shahada ya Udaktari wa Falsafa mhitimu Bakari Ali Mohammed, wakati wa mahafali ya 40 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania yaliofanyika katika Uwanja wa Mao Zedung jijini Zanzibar Wilaya ya Mjini Unguja.

Alikipongeza chuo hicho kwa kufikia malengo ya kuanzishwa kwake ambapo alisema kuwa chuo hicho kina rekodi nzuri katika Afrika kwa kushika nafasi ya kwanza na cha 16 kati ya Vyuo Vikuu Huria 159 duniani na cha 6 kwa ubora miongoni mwa Vyuo Vikuu 54 vya Tanzania

Pia, alitumia fursa hiyo kwa kuwapongeza wahitimu wote kwani anatambua kwamba hatua hiyo haikuwa rahisi bali ni matokea ya jitihada kubwa waliyiofanya hadi kuhitimu kwao na kusema kwamba jamii ina mategemeo makubwa kwao.

Rais Dkt.Mwinyi alisema kuwa, chuo hicho kimekuwa kikiwafikia Watanzania kila kona sambamba na kuwafikia wananfunzi hata walio nje ya Tanzania.

Aidha, alitoa ahadi kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinathamani sana michango ya chuo hicho na zitaendelea kukipa kila aina ya ushirikiano ili kukiwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Rais Dkt. Mwinyi alisema kuwa elimu ya juu ina umuhimu mkubwa wa maendeleo ya nchi kwani hatua hiyo ndiyo inayowajenga vijana na kupatiwa ujuzi muhimu wa kutumikia maendeleo ya nchi.
Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Mhe.Mizengo Peter Pinda akiwatunuku Shahada ya Uzamivu ya Udaktari wa Fasafa (Doctor of Philosophy) wakati wa mahafali ya 40 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania yaliofanyika katika Uwanja wa Mao Zedung jijini Zanzibar, na kulia kwake ni Makamu Mkuu wa Chuo Huria Tanzania, Prof. Elifas Bisanda.

Pamoja na hayo, Rais Dkt.Mwinyi alisema kuwa chuo hicho ni chuo pekee miongoni mwa vyuo vikuu vya Tanzania kilichoweza kuendelea kutoa huduma za kufundisha na kudahili kupitia mtandao bila ya kuathirika na janga la UVIKO-19.

Alieleza umuhimu wa kubuni programu na kozi mbalimbali ili chuo hicho kiendelee kuwa chemchem ya wataalamu mahiri wenye uwezo wa kushindana katika soko la ndani na la Kimataifa.

Alisisistiza haja ya ya kuzingatia mahitaji na vipaumbele vya kupata wataalamu watakaokidhi katika utekelezaji na mipango mikuu ya maendeleo ikiwemo Mpango wa Maendeleo wa Tanzania wa 2025 (Vision 2025), Dira ya Maendeleo ya Zanzibar (2050) pamoja na mipango mengine ya kikanda na Kimataifa.

Akitoa maelezo yake, Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Omar Juma Kipanga alieleza mikakati ya Serikali katika kukiimarisha chuo hicho ikiwa ni pamoja na kuviimarisha vituo vitano hapa nchini kikiwemo kituo cha Pemba.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohammed Said kwa upande wake alisisitiza haja ya kuendelezwa kwa mashirikiano kati ya pande mbili hizi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili maendeleo na mafanikio zaidi yaweze kupatikana.

Nao viongozi wakuu wa Chuo hicho walieleza mafanikio waliyoyapata katika chuo hicho pamoja na changamoto zilizopo.
Wahitimu wa Shahada ya Udaktari wa Falsafa Chuo Kikuu Huria Tanzania wakishangilia baada ya kutunukiwa Shahada yao na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Pinda hayupo pichani, hafla hiyo imefanyika katika uwanja wa Mao Zedung jijini Zanzibar Wilaya ya Mjini Unguja.

Jumla ya wanafunzi 30, wamehitimu Shahada za Uzamivu ya Udaktari wa Falsafa kati ya wahitimu wote 3,110 waliohitimu mwaka huu katika programu na ngazi mbalimbali za Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wakiwepo pia wanafunzi waliohitimu kupitia chuo hicho walioko katika Chuo Kikuu Huria cha Laweh cha nchini Ghana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news