NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi ameishukuru Bodi ya Wakfu wa Benjamin Mkapa (Benjamin Mkapa Foundation-BMF) kwa kuona umuhimu wa kuichagua Zanzibar kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya kumbukumbu ya Rais wa Awamu ya Tatu ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin Mkapa mwaka 2022.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Uongozi wa Wakfu wa Benjamin Mkapa (BMF) ukiongozwa na Mwenyekiti wake kulia kwa Rais, Dkt.Adeline Kimambo, Dkt.Ellen Mkondya Senkoro na Dkt.Ali Uki, walipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu. (Picha na Ikulu).
Dkt.Mwinyi ametoa shukrani hizo Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokuwa na kufanya mazungumza na uongozi wa Bodi ya Wakfu huo, ukiongozwa na Mwenyekiti wake, Dkt.Adeline Kimambo.
Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru taasisi hiyo kwa kazi kubwa inayofanya na kusema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itashirikiana na taasisi hiyo kikamilifu ili kufanikisha maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanyika mwezi Julai 2022, sambamba na kuahidi kuchangia kikamilifu Mfuko wa Wakfu wa taasisi hiyo.
Aliipongeza taasisi hiyo kwa namna inavyotekeleza shughuli zake hapa Zanzibar mbali na kuwepo kwa changamoto za rasilimali.
Alisema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuimarisha sekta ya afya hususan katika uimarishaji wa miundombinu na kubainisha kutumia kikamilifu mkopo iliopata kutokana na fedha za Ugonjwa wa UVIKO-19.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mwenyekiti wa Wakfu wa Benjamin Mkapa, Dkt.Adeline Kimambo kulia kwa Rais alipofia Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu).
Dkt. Mwinyi alipongeza juhudi zinazochukuliwa na wakfu huo katika kuimarisha sekta ya afya na kusema kwamba inathamini michango mbali mbali inayotolewa na taasisi hiyo, ikiwemo upatikanaji wa ajira kwa watumishi wake.
Amesema kuwa, Serikali inakusudia kutengeneza utaratibu utakaowezesha watumishi walioajiriwa na taasisi hiyo kuingia katika mfumo wa Serikali baada ya muda wa utumishi wao kumalizika kulingana na mikataba yao.
Mapema, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Wakfu huo, Dkt. Ellen Mkondya Senkoro alisema maadhimisho ya kumuenzi Hayati Rais Benjamin Mkapa mwaka 2022 yatafanyika Zanzibar, ambapo yataambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo kongamano pamoja na hotuba za Kitaifa.
Alisema, bodi hiyo iko katika hatua za mwisho za maandalizi ya maadhimisho hayo, ikijipanga kutuma maombi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kupata wajumbe watakaoingia katika Kamati ya Maandalizi.
Rasi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Ujumbe wa Wakfu wa Benjamin Mkapa, ukiongozwa na Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Dkt. Adeline Kimambo, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.Picha na Ikulu).
Mtendaji huyo alisema kuanzia mwezi Oktoba mwaka 2021, wakfu huo umeanza utekelezaji wa programu mbalimbali hapa Zanzibar, ikiwemo ya kupambana na maradhi ya UVIKO-19 na Kifua Kikuu.
Alisema taasisi imeajiri wafanyakazi wa kada mbalimbali katika sekta ya afya wapatao 105 Unguja na Pemba ambao wamesambazwa katika vituo 33 vya utoaji huduma, Bandarini na Viwanja vya Ndege, ambapo miongoni mwao watafanyakazi kwa mikataba ya miezi tisa na watumishi watano kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Aidha, alisema taasisi hiyo imeendesha mafunzo mbalimbali kwa watendaji hao ikiwemo ya maadili ya utumishi wa umma, mama na mtoto na UVIKO-19 , huku matokeo ya awali yakionyesha kuwepo mafanikio ya ongezeko la wananchi wanajitokeza kuchanja ugonjwa huo .
Vile vile, alisema tasisi hiyo imekuwa na ushirikiano mkubwa na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto Zanzibar katika nyanja mbali mbali, kwa lengo la kuimarisha sekta ya afya.