Rais Dkt.Mwinyi aushukuru utayari wa Kanisa la Efatha kuunga mkono maendeleo, huduma za kijamii

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amepongeza utayari wa uongozi wa Kanisa la Efatha wa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuleta maendeleo pamoja na kuimarisha huduma za kijamii.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa pongezi hizo leo Novemba 22, 2021 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Kanisa la Efatha lenye Makamo Makuu yake Mwenge jijini Dar es Salaam, ukiongozwa na Kiongozi Mkuu wa kanisa hilo, Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira uliofika Ikulu kwa ajili ya kumpongeza Rais.

Katika maelezo yake, Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, anafarajika kwa kiasi kikubwa pale anapopata watu wa kumuunga mkono katika kuendelza shughuli mbalimbali za maendeleo na kijamii katika kuwahudumia wananchi.

Amesema kuwa,hatua za uongozi wa kanisa hilo la Efatha zinatoa matumaini makubwa katika kuhakikisha kwamba juhudi anazozifanya zimekuwa zikithaminiwa na kuungwa mkono kwani tokea alipoingia madarakani ameshuhudia makundi kadhaa ya kijamii yakiwemo madhehebu ya kidini yameonesha ushirikiano mkubwa kwake pamoja na serikali anayoiongoza.

Amesema kuwa, mafanikio makubwa yameweza kupatikana katika uongozi wake kutokana na wananchi kuwa wamoja na kuweza kuondokana na matabaka katika jamii yakiwemo matabaka ya kidini.

Aliongeza kuwa hatua za Kanisa hilo kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu, afya pamoja na ujenzi wa vituo vya Polisi kuweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuleta maendeleo kwa wananchi na kutoa huduma za kijamii.

Alieleza kwamba kwa vile Zanzibar ni nchi ya utalii hatua za ujenzi wa vituo vya Polisi kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha amani na usalama kwa wananchi pamoja na wageni wanaokuja kuitembelea Zanzibar kwa kuamini kwamba nchi iko salama.
Kwa upande wa sekta ya elimu, Rais Dkt.Mwinyi alieleza kwamba hivi sasa Zanzibar ipo katika hatua za makusudi za kufanya mageuzi ya elimu hivyo, hatua za uongozi huo za kuahidi kushirikiana na Serikali ikiwa ni pamoja na kuwatumia watalamu wake zitasaidia kufikia lengo hilo lililokusudiwa.

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi aliuahidi uongozi huo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari na itaendelea kuweka mazingira mazuri katika kuhakikisha azma inapatikana.

Mapema Kiongozi Mkuu wa kanisa hilo, Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira alimpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa kupata neema ya kuwa Rais wa Zanzibar ambapo ndani ya mwaka mmoja mafanikio makubwa yameweza kupatikana.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuagana na Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Efatha,Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingia, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo.(Picha na Ikulu).

Aidha, Mwingira ambaye amefika Ikulu pamoja na uongozi wa Kanisa hilo kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar, alisema kuwa Rais Dk. Mwinyi kwa vile ana hofu ya Mungu ameweza kuwaunganisha wananchi wa makundi yote bila ya kujali dini, chama, kabila wala jinsia.

Alieleza kuwa utendaji wa Rais Dk. Mwinyi umeweza kufanikiwa kutokana na kiongozi hyo kutokuwa na ubaguzi wa aina yotote ambapo kwa upande wao wakiwa viongozi wa Kanisa la Efatha, wameridhika na juhudi hizo na kuahidi kumuunga mkono yeye na Serikali anayoiongoza ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Kanisa la Efatha, ukiongozwa Kiongozi Mkuu wa kanisa hilo, Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingia (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.

Alifahamisha kuwa, uongozi uliotukuka wa Rais Dk. Mwinyi umepelekea Zanzibar kuwa na umoja ulio imara na kuahidi kwamba uongozi wa Kanisa hilo utaendeleza utamaduni wake wa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta ya elimu, afya, ujenzi wa vituo vya Polisi pamoja na kuendeleza sekta nyengine za maendeleo.

Pamoja na hayo, Kanisa hilo limeahidi kuendelea kuwatumia wataalamu wake katika kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye sekta ya elimu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news