Rais Samia aijaza mamilioni ya fedha timu ya Taifa ya Walemavu

NA MWANDISHI MAALUM

RAIS Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi milioni 150 kwa timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa wenye ulemavu, Tembo Warriors, inayoendelea na maandalizi ya kufuzu Kombe la Dunia kupitia michuano ya Afrika (Canaf) itakayofanyika jijini Dar es Salaam, kuanzia kesho ambapo Tanzania ni mwenyeji.
“Mhe Rais anafahamu mko hapa mnajiandaa kuipigania nchi na amesema nije hapa kwa niaba yake na ametoa kiasi cha shilingi milioni 150 ili kuwawezesha mfanye vizuri zaidi. Simamieni vizuri fedha hizi na mhakikishe zinatumika kama ilivyokusudiwa;

Waziri Mkuu ameyasema hayo Novemba 25, 2021 baada ya kutembelea kambi ya wachezaji wa timu hiyo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. “Viongozi na Watanzania kwa ujumla tuna imani kubwa na timu yetu tunaamini mtafanya vizuri na sisi tutakuja hapa kuwaunga mkono”.

Naye, mlezi wa timu hiyo Mheshimiwa Riziki Lulida ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya maandalizi amesema kwa kuwa Tanzania ni mwenyeji wa mashindano hayo ambayo yatajumuisha timu kutoka nchi 15 za ukanda wa Afrika, ni vyema timu hiyo ikaungwa mkono ili kufanya vizuri na kuwa miongoni mwa timu nne zitakazofuzu katika michuano ya dunia.

Mheshimiwa Riziki ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kutoa fedha hizo na ameahidi kuwa watazitumia vyema ili kuhakikisha timu hiyo inashinda na kuleta heshima kwa Watanzania na hatimaye iweze kufuzu kushiriki michuano ya kimataifa.

Kwa upande wake, nahodha ya timu hiyo, Steven Manumbu, pamoja na kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia pia ametoa ahadi kuwa watajitahidi kuhakikisha wanafanya vizuri katika mashindano hayo ili waweze kushiriki katika mashindano ya dunia ya michezo ya Walemavu.

Waziri Mkuu aliambatana na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Nchi-Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Mhe. Jenister Mhagama, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Venance Mabeyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu-Ofisi ya Waziri Mkuu, Tixon Nzunda, na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news