NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MIRADI ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa nchi nzima imeleta neema na unafuu mkubwa kwa jamii.
Hayo yamebainishwa na Afisa Tarafa ya Mihambwe mkoani Mtwara, Emmanuel Shilatu wakati
alipofanya ziara ya kawaida ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ya elimu
ya ustawi wa jamii kwa Taifa dhidi ya mapambano ya Uviko-19, ambapo
amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu
Hassan kwa kuleta neema kubwa kwa Watanzania kupitia miradi hiyo.
"Kuna wafanyabiashara, wasafirishaji, wauzaji vifaa vya ujenzi madukani, wauzaji vifaa vya kujengea kama vile mawe, kokoto, mchanga na kuendelea, hawa wote wamepata neema ama fursa ya kufanya biashara, kujiongezea kipato kupitia utekelezaji ujenzi miradi hii ya elimu na mengineyo.
"Hivyo kwa niaba ya wananchi wa Tarafa ya Mihambwe tunamshukuru sana Rais Samia kwa miradi
hii inayoenda kuondoa uhaba wa madarasa na pia amefanya mzunguko wa
fedha uongezeke kwa jamii ambapo miradi hiyo inatekelezwa,"amesema
Gavana Shilatu.
Gavana Shilatu pia alitumia ziara hiyo kuwasisitiza mafundi kuongeza kasi zaidi ya ujenzi, kamati za miradi kuhakikisha wanasimamia ubora wa vifaa na ujenzi ili miradi ikamilike kwa wakati, kwa ubora unaolingana na thamani ya fedha.
Tarafa ya Mihambwe imepata fedha toka Serikali Kuu shilingi milioni 420 kujenga vyumba vya madarasa 19 kwa shule za sekondari tano na vyumba madarasa mawili kwa shule shikizi moja.
Katika fedha hizo hizo pia wanajenga ofisi tisa za walimu na kuweka viti na meza kwenye madarasa hayo yote 21.