NA MWANDISHI MAALUM
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imeamua kuruhusu wanafunzi wote walioacha shule kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro, sababu za kisheria au walioshindwa kufaulu darasa la saba kupewa nafasi nyingine ya kuendelea na masomo.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2021/11/7-15.jpg)
Amesema, lengo la maamuzi hayo ya Serikali ni kutoa fursa pana kwa watoto wa kitanzania kuweza kuendelea na elimu ili iweze kuwasaidia katika maisha.
Mhe. Rais Samia amesema hayo Novemba 29, 2021 katika hafla ya makabidhiano ya Shule ya Awali na Msingi Museveni iliyokabidhiwa kwakwe na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, katika kijiji cha Nyabilezi, Chato mkoani Geita.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2021/11/4-42-scaled.jpg)
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema kwa wanafunzi watakaoshindwa kuendelea na mfumo wa masomo wa kawaida wanaweza kujiunga na Elimu Mbadala ambayo itawezesha kujitegemea kimaisha kwa kuwa inatoa stadi mbalimbali za maisha kama ilivyo katika baadhi ya nchi.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2021/11/5-32-scaled.jpg)
Pia, Mhe. Rais Samia amesema makabidhiano ya Shule hiyo iliyogharimu jumla ya Dola za Marekani Milioni 1.67, yamefanyika wakati muafaka ambapo itaongeza fursa kwa wanafunzi wote kupata elimu hata kwa wale wenye mahitaji maalum.
Mhe. Rais Samia amemshukuru Rais Museveni kwa wema na utu wake na kujitoa kuhakikisha kuwa elimu bora sio suala la mipaka ila ni jukumu la viongozi wote wa Afrika katika kusaidia bara letu kutoa elimu bora na yenye viwango ili kuweza kukidhi soko la ajira.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2021/11/8-13-scaled.jpg)
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema majengo ya shule hiyo yatabaki kama alama ya kipekee katika kumbukumbu za watanzania na wanachato kwa ujumla na ndio maana Serikali ikaamua kuisajili shule hiyo kwa jina la Mhe. Rais Museveni na itajulikana kama Shule ya Msingi Museveni na itafundisha kwa mtaala wa Kingereza.
Vilevile, Mhe. Rais Samia amewataka wanafunzi watakaopata nafasi ya kujiunga na Shule hiyo kutumia fursa wanayoipata kujifunza kwa bidii ili waweze kufanya vizuri kwenye masomo yao na elimu watakayoipata iweze kuwasaidia katika maisha yao ya baadae.
Katika kuenzi mchango wa Rais Museveni na Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Mhe. Rais Samia ameiagiza Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kuweka historia ya Marais hao kwenye Maktaba yake ili kusaidia wanafunzi watakaosoma shuleni hapo kujifunza uzalendo, umajumui na falsafa za Marais hao ili kuhakikisha waafrika wanajitegemea kwenye sekta za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2021/11/6-23-scaled.jpg)
Serikali ya Tanzania imetoa Shilingi milioni 705,000,000 kwa ajili ya ununuzi wa samani na ukamilishaji wa kazi za nje ambazo hazikuwa sehemu ya mkataba wa ujenzi wa Shule hiyo na inatarajiwa kuchukua wanafunzi 630 wa Bweni itakapokamilika.
Shule hiyo ya Awali na Msingi ina vyumba vya madarasa ya Shule ya Msingi 17, Maktaba 1, vyumba vya madarasa ya Elimu ya Awali 3, Jengo la Utawala 1, Ofisi kwa ajili ya Elimu ya Awali 2, Matundu ya vyoo 37 na Nyumba ya Walimu.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2021/11/20-1-scaled.jpg)
Mhe. Rais Museveni amemaliza ziara yake ya Kitaifa ya siku tatu hapa nchini ambapo ameagwa rasmi na Mhe. Rais Samia katika Uwanja wa Ndege wa Geita uliopo wilayani Chato mkoani humo.