NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kesho Novemba 10, 2021 anatarajiwa kuondoka nchini kuelekea Cairo nchini Misri kwa ziara ya Kiserikali ya siku tatu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Jaffar Haniu iliyotolewa leo Novemba 9, 2021 ziara hiyo ya Kiserikali ya siku tatu inafuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Mhe. Abdel Fattah Al Sisi.
Katika ziara hiyo, Mhe. Rais Samia pamoja na mambo mengine anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake katika maeneo kadhaa ya ushirikiano kati ya Tanzania na Misri ikiwemo nyanja za diplomasia, uchumi, siasa, elimu, utalii na huduma za kijamii.
Mhe. Rais Samia na mwenyeji wake pia wanatarajiwa kushuhudia utiaji saini mkataba mmoja (1) na hati saba (7) za makubaliano kati ya Tanzania na Misri.
Tags
Habari