NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila amesema kwamba taasisi za dini zina mchango mkubwa sana katika kuhakikisha amani, utulivu na uimara wa Taifa letu na ndio sababu Serikali ya Tanzania katika awamu zote imefanya taasisi za dini kuwa mdau muhimu wa maendeleo na utengamano wa Taifa letu.
Mtumishi wa Mungu, Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila wakati wa uzinduzi wa jengo la ibada la Kanisa la Efatha Simiyu. Uzinduzi wa jengo la Kanisa la Efatha Simiyu umefanyika Novemba 11, 2021 pamoja na kukabidhi cheti cha kuwa kanisa kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo kusimika viongozi mbalimbali katika kanisa hilo.
"Kazi ya kwanza ya Serikali yoyote duniani ni kuhakikisha usalama na utengamano wa Taifa husika. Nikuhakikisha Taifa ni moja na watu wake wote wanajiona hivyo. Hii sio kazi ya kawaida. Ni kazi kubwa, endelevu na ya kudumu.
"Hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana kwenye Taifa vipande vipande. Viongozi wa dini mnapaswa kuendelea kusaidia hilo.
"Dini inajenga ustaarabu wa mwanadamu. Ni gharama kubwa kuongoza Taifa la watu wasio wastaarabu. Duniani leo ushindani ni ubora wa nguvu kazi yaani human capital, sio tena maliasili. Nguvu kazi hii inapimwa zaidi katika mambo matatu mbali ya afya ya mwili. Inapimwa kwa bidii, maarifa na uadilifu.
"Hizo ndio sifa tatu zinazoamua ushindani wa nguvu kazi duniani. Dini inasisitiza uadilifu na bidii, dini inasisitiza elimu. Nimalizie kusema taasisi za dini zina umuhimu mkubwa pengine kuliko hata vyama vya siasa, na kama isingekuwa kusema kazi dini watalipwa na Mungu wangeweza kustahili ruzuku ili watoe huduma.
"Leo Serikali duniani zinatumia sehemu kubwa ya kodi kugharimia majeshi kwa sababu kuna binadamu wengi hatufuati amri za Mungu. Lakini tungefuata amri za Mungu ajira zote za majeshi zingekuwa za sekta zingine Elimu-, Afya, Kilimo na uhandisi,"amesisitiza Mheshimiwa Kafulila katika hotuba yake Novemba 11, 2021 wakati wa uzinduzi wa Kanisa la EFATHA mkoa wa Simiyu uliongozwa na Nabii na Mtume na Nabii Josephat Mwingira.