NA DOREEN ALOYCE
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa, rushwa ya ngono inakoma kabisa chuoni hapo.
Profesa Bernadeta Lillian ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo (Utafiti) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akielezea kuhusiana na kongamano la tatu la utafiti kwa maendeleo jumuishi ambalo litafanyika jijini hapa kesho.
Kongamano ambalo linawakutanisha pamoja wadau wa waendeleo, watafiti na wanataaluma kutoka katika nyanja mbalimbali, lengo likiwa ni kujadili kwa pamoja jinsi ya kuboresha maisha ya watanzania na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Profesa huyo ameyasema hayo baada ya kuulizwa swali juu ya taarifa ya rushwa ya ngono katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na tafiti zinasemaje juu ta tatizo hilo.
Amesema, ni kweli tatizo hilo lipo chuoni hapo, lakini wamekuwa wakikabiliana nalo kwa kujiwekea sheria mbalimbali za kinidhamu.
"Katika chuo chetu tataizo la rushwa ya ngono lipo, lakini tumekuwa tukikabiliana nalo kwanza kabisa chuo chetu kimekuwa kikiongozwa kwa sera mbalimbali zinazohusiana na masuala ya kijinsia na tumekuwa tukiwafuatilia wanafunzi na waadhiri lengo likiwa ni kuhakikisha nidhamu inatawala chuoni hapa.
"Wapo watumishi ambao tumeshawafukuza kazi kutokana na kubainika kujihusisha katika vitendo hivyo katika chuo chetu cha Dar es Salaam pia tumekuwa tukiwapa elimu ya kijinsia wanafunzi wote wanaoingia mwaka wa kwanza chuoni ili waweze kujitambua," Profesa Bernadeta amebainisha.