Serikali kufufua kiwanda cha kuchakata mafuta ya mawese cha Trolle Meesle Tanzania Limited mkoani Kigoma

NA DOREEN ALOYCE

KATIKA jitihada za kukuza uchumi wa viwanda hapa nchini, Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema Serikali imedhamiria kufufua mradi wa kiwanda cha kuchakata mafuta ya mawese kijulikanacho Trolle Meesle Tanzania Limited kilichopo mkoani Kigoma.
Aidha, kiwanda hicho kilichopo Mtaa wa Sido mkoani Kigoma kilisimama takribani miaka sita jambo ambalo lilipelekea vijana wengi kukosa ajira na hata Serikali kushindwa kupata Pato la Taifa linalotokana na malighafi hizo.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma Novemba 17,2021 mara baada kumalizika mazungumzo baina ya Serikali na wadau ambao ni wafadhili wa kiwanda hicho ikiwemo Benki ya CRDB ambayo imeonyesha nia ya kutoa kiasi cha fedha bilioni 1.2 kwa ajili ya kufufua kiwanda hicho.

"Nipende kuwataarifu watanzania kwamba hivi karibuni uzalishaji wa malighafi unaotokana na kiwanda hicho utaanza mara moja na hiyo ni kutokana na agizo la Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa alilolitoa kwa Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda alipokuwa ziarani huko Kigoma na uzuri Benki ya CRDB ambayo wameonyesha nia ya kufadhili mradi huo ikiwemo wakulima mabao wataingia katika Chama cha Ushirika (AMCOS)," amesema Bashe.

Ameongeza kuwa, mradi huo hapo awali ulikuwa chini ya Kampuni ya Primasli na kufadhiliwa na Ubalozi wa Denmark kupitia shirika lake la maendeleo la DANIDA kwa kushirikiana na Serikali ambapo ulikamilika mwaka 2019.

"Kulikuwepo na makubaliano ya kisheria katika uwekezaji huo na kiasi cha shilingi milioni 450 kama dhamana ambayo ni fedha waliyokopa,waliweka ya mali zisizohamishika ikiwemo nyumba na vitu vyake ,ambavyo vifaa vyote vilifika na hivi sasa mashine zote za kuweza kuchakata mafuta ya mawese ziko mkoani Kigoma toka mwaka 2019 katika ofisi za SIDO,"amesema Bashe.

Akielezea chanzo cha kukwamisha kuanza mradi huo amesema kuwa, ni mambo ya ukamilishwaji hasa gharama ya ufungaji mashine na mtaji Ili kiwanda kiweze kufanya kazi ambapo kina uwezo wa kuzalisha tani 24 kwa siku.

Aidha, Bashe ameongeza kuwa katika kufanikisja zoezi hilo watafanya kikao cha pili ambacho kitahusisha benki ya CRDB, TADB, Ubalozi wa Denmark kwa maana ya DANIDA,uongozi wa Mkoa wa Kigoma ,Wizara ya Kilimo na mwekezaji aliyechukua mkopo wa shilingi milioni 450 kuweza kukamilisha mradi huo.

Hata hivyo amesema kuwa, katika makubaliano ya pande zote hizo zikakae na kila mmoja kurekebisha katika eneo lake ,dhamira yao kabla ya Machi mwakani mabapo mradi huo uwe umeanza kufungwa kwa mashine na uchakataji wa mafuta ya mawese uanze katika Mkoa wa Kigoma.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kiwanda hicho, Abdul Mwilima alisema kitendo cha Serikali kufufua kiwanda hicho itakuwa mkombozi kwa wakulima wa mchikichi zaidi ya watu 300 ambao watapata soko la uhakika.

Pia amesema itasaidia kuhamasisha kuongeza uzalishaji wa mazao hayo na kuokoa pesa nyingi za kigeni ambazo utumika kununua mafuta nje ya nchi kutokana na uhaba wa mafuta uliopo hapa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news