NA NTEGHENJWA HOSSEAH, OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Ummy Mwalimu amemuagiza Katibu Mkuu Profesa Riziki Shemdoe kupitia upya orodha ya mahitaji ya shule ili kuondoa mahitaji yasiyo ya lazima ambayo ni kikwazo kwa wanafunzi kuripoti shuleni.
Mhe. Ummy alitoa agizo hilo Novemba 24,2021 wakati wa kutangaza wanafunzi waliochanguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022.
Amesema, kumekuwa na tabia ya shule kutoa orodha ya mahitaji ambayo si ya lazima na yamekuwa kikwazo kwa wanafunzi kwenda shule.
Aidha, Mheshimiwa Ummy pia amewaagiza wakuu wa mikoa, wilaya, viongozi na watendaji wa halmashauri kuhakikisha kwamba wanaondoa vikwazo visivyo vya lazima kwa ajili ya wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza.
"Kumekuwa na utaratibu mwingine wa ajabu, utasikia kwenye join instruction ( fomu ya kujiunga) sijui uje na kitu hiki au kile ambacho hata hakina umuhimu wa moja kwa moja, uje na rimu sijui.
"Mara njoo na track suti jozi mbili, anaweza kuja na moja nyingine akanunua hapo baadaye kwa sababu mzazi kwa muda huo hana fedha watoto wengine wanatoka kwenye kaya zenye kipato cha chini zaidi. Kwa hiyo jukumu letu kama viongozi kuondoa vikwanzo vyote visivyo vya lazima kwa watoto na ndio maana nimemuelekeza Katibu Mkuu kupitia orodha ya mahitaji ili yale ambayo si ya lazima yaondolewe,"amesema Waziri Ummy.a
Ameongeza kuwa, "natamani sana baada ya shule kufunguliwa watoto wote niweze kuwaona kama siwezi kuwaona watoto wote 907,802 basi nitawaona shule za binafsi,lakini tunatamani tusipoteze mtoto hata mmoja ambaye amefaualu na tumepangia shule,"amesema.
Aidha, Waziri Ummy alitoa rai kwa wazazi kuhakikisha watoto wao wanakwenda kuripoti shule kwani Serikali inaweka mazingira wenzeshi ya watoto kuendelea na masomo ya sekondari.