Serikali yadhamiria kuimarisha mfumo wa utoaji huduma za ustawi wa jamii nchini

NA MWANDISHI MAALUM

SERIKALI imesema kuwa, itaendelea kuimarisha mfumo wa utoaji huduma za ustawi wa jamii nchini ili kuhakikish haki za watu wenye mahitaji maalumu walio pembezoni wanapata huduma zote za msingi kwa wakati.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Siku Nne na Mkutano Mkuu wa wataalamu na watoa huduma za ustawi wa jamii linalofanyika katika ukumbi wa Benki ya Tanzania (BoT) Mwanza kuanzia Novemba 24 hadi 27, Novemba 2021

Amesema, wanatambua kwamba Chama cha Wataalamu wa Ustawi wa Jamii kimekuwa kikifanya kazi kwa karibu na serikali kwa kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto, Wazee na Watoto, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) pamoja na wadau wengine wa maendeleo katika kutatua changamoto mbalimbali zinazokwamisha utoaji wa huduma bora za ustawi wa jamii.

“Wizara yangu inatambua mchango mkubwa wa TASWO katika kusimamia na kutetea haki za wanataaluma, watoa huduma pamoja na makundi nufaika ya huduma za ustawi wa jamii hapa nchini,"amesema Dkt.Gwajima.

Katika mkutano huo uliobebwa na kauli Mbiu “UBUNTU” neno lenye maana ya “I AM because WE ARE” alisema kauli mbiu hii iwasaidie kukuza mahusiano baina yao na kusaidia kuwaweka watoa huduma na wanufaika na huduma karibu hivyo kutoa fursa ya kujenga mshikamano kwa ajili ya kupanga namna ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili jamii.

Aidha aliwapongeza Maafisa Ustawi wa Jamii katika ngazi zote za utoaji wa huduma kwa umahiri mkubwa wanaounyesha na kwa jitihada mnazochukua kushughulikia changamoto na matatizo mbalimbali ya masuala ya migogoro ya ndoa na familia, huduma kwa wazee na watu wenye ulemavu, ukiukwaji wa haki za watoto pamoja na ukatili wa kijinsia. “Ninatambua kuwa, Wataalamu wa Ustawi wa Jamii wanafanyakazi kubwa sana katika Idara ya Afya kupitia vituo vya afya, hospitali za wilaya ,hospitali za mikoa pamoja na hospitali za rufaa,"ameongeza Dkt.Gwajima.

Alisema, maafisa hao hutumika kutoa huduma za msaada wa kisaikolojia na ushauri nasaha kabla na baada ya matibabu, maelekezo ya namna ya kujikinga na maambukizi zaidi ya magonjwa, kushiriki kampeni za elimu kwa umma, ufuatiliaji na tafiti za kijamii kwalengo la kutoa huduma bora za afya kwa wahitaji, utambuzi na usimamizi wa huduma za msamaha kwa wagonjwa na wazee.

Akizungumzia lengo la Kongamano hilo Mwenyekiti wa TASWO nchini Dkt.Mariana Makuu alisema ni kuwakutanisha wananchama nchi nzima ni sehemu ya kukutana na kuongea kwa pamoja ambayo yanatekelezwa na maafisa ustawi katika maeneo yote.

“Zaidi ya Wanachama 300 tumekutana leo kwa ajili ya kuongea kwa pamoja yale yanayotekelezwa na maafisa ustawi katika maeneo yote kuhakikisha kwamba wanatoa huduma kwa jamii na makundi maalumu pamoja na kuainisha changamoto wanazokutana nazo kwa lengo la kuona ni mkakati gani ambao unaweza kutumika kutatua matatizo hayo,"amesema Dkt.Mariana.

Mbali na lengo hilo pia alizungumzia changamoto mbalimbali kwenye sekta yao ikiwemo kutokuwepo kwa ofisi za kutosha kwa ajili ya kufanyia shughuli zao na hivyo kuiomba Serikali kama itawezekana kuwepo na ofisi ambazo watakuwa wakizitumia bila kuchanganywa na idara nyingine.

“Maeneo ya kufanyia kazi kama ustawi wa jamii sio rafiki afisa hana ofisi yake peke yake unakuta wamekaa kama timu, na unapoingia unaingia kwa daktari wa jamii na afisa anahitaji kuchimba ili ajue tatizo sasa wewe ukiwa na tatizo huwezi kulitoa katika mazingira hayo,"aliongeza Dkt.Mariana.

Aidha, alisema mkutano huo ambao hufanyika kila mwaka na kupitia mikutano hiyo hukutana na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, wadau wa maendeleo.

Afisa Ustawi wa jamii kutoka Mkoani Mwanza Bi Faithmary Lukindo aliiomba Serikali kuajiri maafisa ustawi wengi Zaidi ili waendelee kutoa huduma kwa jamii, huku Bw Peter Misaka Afisa Ustawi kutoka Mkoani Kilimanjaro akiiomba Serikali iongeze bajeti kwa maafisa ustawi.

“ Kikubwa ni kama alivyosema Mhe Waziri kuna upungufu wa wataalanu wa ustawi wa jamii kwa 80% kwenye ngazi ya kata na 60% kwenye ngazi ya Halmashauri za Wilaya sisi ombi letu Serikali itoe ajira mpya kwa maafisa wengi zaidi ili tuendelee kuhudumia jamii pamoja na kutatua changamoto zao,"amesema Bi.Lukindo. Akijibu Ombi hilo waziri Gwajima alisema Wizara yake imeendelea kuomba vibali vya ajira kwa ajili ya kupunguza tatizo lililopo na kufika huduma stahiki kwa wanajamii nchini.

“Ni kweli kuna uhaba wa Maafisa Ustawi wa Jamii, hata hivyo, Wizara imeendelea kuomba vibali vya ajira hivyo, kadiri tutakavyopatiwa watumishi wapya, wizara yangu itawapangia kazi katika maeneo na vituo vyenye uhitaji zaidi kwa lengo la kuboresha huduma,"amesema Dkt.Gwajima.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt.Thomas Rutachunzibwa aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi aliitaja kada ya Ustawi wa Jamii kuwa ni moja wapo ya nguzo muhimu sana katika kusaidia jamii hasa yanapotokea majanga makubwa yanayolikumba Taifa akitolea mfano tetemeko lililowahi kutoka Mkoani Kagera .

“Ndugu Mgeni Rasmi kama utakumbuka nchi yetu ilikumbwa na janga la tetemeko mimi nilishiriki nikiwa mmoja wao nilishuhudia kazi kubwa ya ustawi wa jamii, na kama haitoshi wakati wa kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere kule Bwisya, hawa watu walifanya kazi kubwa sana sasa hayo matukio yameniongezea wigo mkubwa wa kutambua umuhimu wa wataalamu wa ustawi wa jamii kwa kiwango kikubwa sana,"amesema Dkt.Rutachunzibwa.

Mkutano huo wa siku nne( unawakutanisha Wawakilishi wa Mashirika na Wadau wa huduma za ustawi wa jamii kama UNICEF, ABBOT FUND, PACT, SOS VILLAGES, Viongozi wa TASWO, Waadhiri wa vyuo vikuu vinavyozalisha Wataalamu wa Ustawi wa Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Mikoa ya Tanzania Bara, visiwani na Wadau na Watoa huduma za Ustawi wa Jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news